• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
FATAKI: Ikiwa wewe bahili wa mali na moyo, basi mapenzi yatazidi kukuchenga

FATAKI: Ikiwa wewe bahili wa mali na moyo, basi mapenzi yatazidi kukuchenga

Na PAULINE ONGAJI

MAJUMA kadhaa yaliyopita nilizungumzia kuhusu kikundi fulani cha wanaume cha kubuni mtandaoni kinachojiita Stingy Men Association, ambacho kulingana na wanachama wake, ni ili kuhakikisha kwamba hakuna mwanamume anayegharimia mahitaji ya mwanamke.

Japo nilisisitiza kwamba kikundi hiki ni cha matani tu, suala la wanaume bahili limekuwa likijitokeza mara kwa mara miongoni mwa mabinti. Nakumbuka nilisema kwamba hakuna mwanamune bahili, na suala kuu ni iwapo kaka anakupenda au hakupendi.

Nakumbuka pia nikisema kwamba mwanamume akikupenda atahakikisha kwamba una chochote unachohitaji, na hata ikiwa hana uwezo wa kifedha, atajitahidi angaa kuhakikisha anatafuta mbinu za kukidhi hitaji lako kwa njia moja au nyingine.

Ni sawa na suala la mapenzi na kugawa asali miongoni wanawake. Hata kwa muktadha wa mabinti, penzi ni lile lile. Hakuna mwanamke rahisi au mgumu kimapenzi.Hakuna mwanamke bahili kimahaba na ikiwa anafanya hivyo, basi huenda hakupendi, au huna rasilimali za kumuondolea njaa yake. Njaa hii yaweza kuwa ya kifedha, ya kirasilimali, kitaaluma, kielimu au ya hadhi, kuambatana na mahitaji au tamaa yake.

Kuna mabinti wanaopenda kwa tumbo ambapo aina ya njaa aliyo nayo, itamchochea akupe penzi au la. Je, una fedha za kutosha kumuondolea umaskini? Je, hadhi yako ni ya juu kiwango cha kumuinua pia yeye? Je, unaweza muinua kielimu?

Maswali mengi vipusa wa aina hii hujiuliza ni ikiwa mahitaji yake ya kifedha yatashughulikiwa, iwapo utamuinua au kumpandisha hadhi katika jamii.

Ikiwa wewe ni kaka mwenye uwezo wa kumuondolea binti anayesukumwa na tumbo njaa yoyote kati ya hizi, amini usiamini, hata hutoitisha uhondo mara mbili.

Kwa upande mwingine, kunao wanaopenda kwa moyo kumaanisha penzi la dhati na kweli. Huyu ni mwanamke ambaye penzi lake kwako lina uwezo wa kumyeyusha kimahaba na hatosita kukufungulia kibuyu cha asali. Huyu ni binti ambaye uwe tajiri au maskini, mradi amekupenda, atakupa moyo wake wote bila kusita.

Hivyo basi dhana ya mwanamke mgumu au mwepesi kimahaba ni suala la kujadiliwa. Kwa mwanamke anayekupenda, penzi lako latosha kuyeyusha kuta za moyo wake hata bila kutoa kijasho. Ikiwa ni yule anayesukumwa na tumbo, ukiwa na rasilimali za kushibisha njaa aliyo nayo, vile vile hautakuwa na kibarua kigumu kumtwaa. Lakini ikiwa hauna chochote kati ya hivi na haujauteka moyo wa binti, jaribio lako la kutaka kumtwaa ni sawa na kukamua jiwe kavu likupe maji.

You can share this post!

UMBEA: Kukutana na mtu mnayeendana ni kibarua ila...

Marudio ya uchaguzi wa viongozi wa GTMA yafanyika kwa amani...