Presha ya kazi ya ukocha ni kama oksijeni kwangu – Mourinho

Na MASHIRIKA

MKUFUNZI Jose Mourinho wa Tottenham Hotspur amesema presha ya kuhifadhi kazi yake kwa sasa ni kama oksijeni ambayo ni kiini cha maisha yake.

Mbinu za kocha huyo raia wa Ureno zimekuwa zikikosolewa mara kwa mara na mashabiki msimu huu baada ya waajiri wake kupoteza jumla ya mechi tano kati ya sita kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Matokeo hayo yaliwatupa Spurs hadi nafasi ya tisa jedwalini kwa alama 36 sawa na Aston Villa huku wakiwa sasa katika hatari ya kupitwa na Leeds United, Arsenal, Wolves na Crystal Palace.

Akijohiwa na wanahabari mnamo Ijumaa, Mourinho alisema kwamba wakati wa pekee ambapo amewahi kuhisi presha ni kipindi ambapo hakuwa na kazi kwa takriban mwaka mmoja kabla ya Tottenham kumwajiri mnamo Novemba 2019.

“Matatizo katika taaluma ya ukocha huanza wakati ambapo mkufunzi hana presha. Kwangu presha ni sawa na oksijeni, ndiyo maisha,” akasema mkufunzi huyo wa zamani wa Manchester United, Real Madrid na Chelsea.

Tottenham kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Burnley mnamo Februari 28, 2021 na ushindi utawawezesha kuwakaribia mabingwa watetezi Liverpool ambao wamejizolea jumla ya alama 40 kutokana na mechi 25 zilizopita.

Ni pengo la alama saba ndilo linatamalaki kati ya Spurs na West Ham United ambao kwa sasa wanafunga orodha ya tano-bora kwa alama 43.

Huku matumaini ya kukamilisha kampeni za EPL msimu huu ndani ya orodha ya nne-bora yakididimia, njia nyingine ambayo Spurs wanaweza kutumia ili kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao ni kutia kapuni ufalme wa Europa League. Kikosi hicho kimepangiwa kuvaana na Dinamo Zagreb ya Croatia kwenye hatua ya 16-bora ya kivumbi hicho msimu huu.

Spurs pia wamepangiwa kuchuana na Manchester City kwenye fainali ya Carabao Cup itakayochezewa uwanjani Wembley, Uingereza mnamo Aprili 25, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO