Raila mbioni kuzima injili ya Ruto kuhusu BBI

MOHAMED AHMED na SHABAN MAKOKHA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga amepanga msururu wa mikutano wiki hii kuvumisha mswada wa marekebisho ya katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI).

Wiki moja baada ya mabunge mengi ya kaunti kupitisha mswada huo, Bw Odinga amepanga kuzuru maeneo ya magharibi na Pwani kupigia debe kura ya maamuzi.

Maeneo hayo mawili ni miongoni mwa yale ambayo Naibu Rais William Ruto na kikosi chake wamezuru mara nyingi kujaribu kushawishi wananchi dhidi ya kuunga mkono BBI.

Gavana wa Busia, Bw Sospeter Ojaamong alisema ataungana na wakazi wa kaunti hiyo kumshinikiza kiongozi wake wa chama cha ODM awasilishe pendekezo lao la kutaka kuongezewa maeneobunge.

“BBI imependekeza pabuniwe maeneobunge mapya 70, lakini Busia si miongoni mwa kaunti zitakazonufaika. Tungependa kuongezwa maeneobunge. Ninaomba wakazi wangu wampokee vyema waziri mkuu wa zamani. Akikubali pendekezo letu tutamshukuru Mungu,” akasema Bw Ojaamong.

Alikuwa akizungumza Ijumaa katika eneo la Teso Kaskazini wakati wa mazishi ya naibu mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Kamumuoit, marehemu Hellen Okumu.

Bw Odinga anatarajiwa kuhudhuria ibada katika Kanisa Katoliki la Lwanya leo asubuhi, kisha akitoka hapo atakutana na viongozi wa kaunti hiyo katika hoteli ya Bukalama Resort na baadaye atafanya mikutano ya hadhara mjini Busia.

Kiongozi huyo anarajiwa kuzuru kaunti za Taita Taveta na Kwale na kumalizia Mombasa ndani ya wiki hii.

Ziara hiyo ya Pwani inakuja wakati ambapo pia chama chake kinakumbana na msukosuko unaosababishwa na wandani wake wa chama, magavana Hassan Joho na Amason Kingi.

Magavana hao wawili wamekuwa wakikitishia chama cha ODM huku Bw Kingi akisema kuwa kuna haja ya Pwani kujiondoa chamani humo naye Bw Joho akisema anataka kuungwa mkono na Bw Odinga.

Mivutano hiyo inahofiwa kuwa itampa Naibu Rais William Ruto nafasi bora ya kupenya eneo hilo, ilhali Bw Odinga anahitaji uungwaji mkono kupitisha BBI kabla ya kutafutia ODM kura za urais hapo baadaye.

Katika ziara yake, Bw Odinga anatarajiwa kufanya mikutano kadhaa ambayo miongoni mwa mambo mengine, atashirikisha mazungumzo hayo ya Pwani kutaka kuunda chama chake.

Kulingana na wadokezi wa Taifa Jumapili, Bw Odinga atafanya mkutano mkubwa Mombasa baada kuzunguka sehemu za kaunti hizo nyingine.

Ziara ya Bw Odinga inakuja wiki kadha baada ya Dkt Ruto kuzuru eneo hilo. Dkt Ruto pia ameonakana kumtatiza Bw Odinga kufuatia ziara hizo zake za Pwani ambapo tayari ana ufuasi ijapokuwa ni mdogo sana kwa sasa.

Kufikia sasa Dkt Ruto ameshikilia viongozi wa Kwale na wengine wachache kutoka kaunti ya Kilifi.

Baadhi ya viongozi ambao wanamuunga mkono Dkt Ruto ni wabunge Aisha Jumwa (Malindi), Owen Baya (Kilifi Kaskazini), Paul Katana (Kaloleni).

Wengine ni Gavana Salim Mvurya, mbunge wa Kinango Benjamin Tayari na mwenzake wa Lunga Lunga Khatib Mwashetani.

Habari zinazohusiana na hii

UHURU AMTULIZA RAILA

Wababaisha ‘Baba’

ODM: Raila anachezwa

Kingi amzima Raila

Kichwa kinauma

Raila akausha marafiki