Raia waumia siasa zikivuma

Na VALENTINE OBARA

HALI ya maisha kwa Wakenya inaendelea kuwa ngumu huku viongozi wenye jukumu la kupitisha sera za kuboresha hali hiyo wakijikita katika kupiga domo la kisiasa.

Ripoti kuhusu bei ya bidhaa na mfumko wa gharama kiuchumi iliyotolewa Jumamosi na Idara ya Takwimu za Kitaifa (KNBS), imeonyesha kuwa bidhaa nyingi na huduma zinazotegemewa kila siku na mwananchi wa kawaida zinaendelea kuwa ghali kila kukicha.

Hayo yanajiri wakati ambapo siasa kuhusu urekebishaji katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) na uchaguzi wa urais 2022 zimepewa kipaumbele na viongozi wengi.

Kwa mujibu wa KNBS, bidhaa muhimu kama vile mafuta ya kupikia, sukumawiki, mafuta ya petroli na dizeli zilipanda bei Februari ikilinganishwa na ilivyokuwa Januari. Wakati huo huo, nauli pia ilipanda.

Bei ya unga wa ngano, mfuko wa kilo mbili, ilipanda kutoka Sh125.64 hadi Sh128.24 kwa wastani.

Hali sawa na hii imekumba bei ya nyama ambayo kilo moja imepanda kutoka Sh455.44 hadi Sh459, huku bei ya sukuma wiki ikipanda kutoka Sh50.71 hadi Sh51.71, spinachi kutoka Sh55.77 hadi Sh58.22 na kabichi kutoka Sh39.15 hadi Sh40.87 kwa kilo moja.

Ripoti hiyo iliyotiwa sahihi na Mkurugenzi Mkuu wa KNBS, Bw McDonald Obudho, inaonyesha kuwa bei ya nyanya kilo moja ilipanda kutoka Sh95.40 hadi Sh97.41, huku bei ya mafuta ya kupikia ikipanda kutoka Sh227.66 hadi Sh236.45.

“Kwa jumla, mfumko wa bei ya vyakula na vinywaji ilipanda kwa asilimia 1.01 kati ya Januari 2021 na Februari 2021. Mfumko huu ulisababishwa na ongezeko la bei ya baadhi ya vyakula, ambapo kiwango cha ongezeko kilikuwa juu kuliko kiwango cha bidhaa zilizopungua bei katika kipindi hicho,” akaeleza Bw Obudho.

Miongoni mwa bidhaa ambazo zilishuka bei kidogo ni mahindi na bei ya umeme.

Gharama ya maisha ilianza kulemea Wakenya wengi tangu ugonjwa wa Covid-19 ulipothibitishwa kuingia nchini mnamo Machi mwaka uliopita.

Kanuni zilizobuniwa ili kudhibiti ueneaji wa maambukizi ya virusi vya corona nchini na kimataifa zilisababisha pigo kubwa kwa biashara ambayo matokeo yake ni kuwa watu wengi walibaki bila ajira huku wengine wakipunguziwa mishahara.

Rais Uhuru Kenyatta anasubiriwa kutangaza ikiwa baadhi ya kanuni zilizopo zitalegezwa, kuendelezwa au kukazwa zaidi baadaye mwezi ujao.

Licha ya hali hii kuwepo, viongozi wamekuwa wakikosolewa kwa kutilia maanani siasa za BBI na urithi wa urais badala ya kutumia muda wao mwingi kutafuta suluhisho na jinsi ya kufufua uchumi haraka iwezekanavyo.

Wiki hii, mabishano kuhusu mswada wa marekebisho ya katiba (BBI) yanatarajiwa kuelekea katika Bunge la Taifa na Seneti.

Spika wa Seneti, Bw Kenneth Lusaka jana alisema wamepokea ripoti kutoka kwa mabunge ya kaunti 38 yaliyopitisha mswada huo.

Kulingana na Kiongozi wa chama cha ANC, Bw Musalia Mudavadi, suala la BBI limedumu kwa muda mrefu kupita kiasi na linafaa kutamatishwa ili changamoto zinazokumba wananchi zitatuliwe haraka.

“Mzigo mzito kitaifa si kuhusu BBI. Hilo ni suala la kisiasa ambalo hatuwezi kuliepuka, lakini tunafaa kutilia maanani suala la uchumi.

Tunafaa tutafute jinsi tunavyoweza kusaidia Wakenya kupata nafasi za ajira,” akasema Bw Mudavadi katika mahojiano ya redio mnamo Ijumaa.

Urithi wa Rais Kenyatta atakapostaafu mwaka wa 2022 pia umetikisa serikali kwa kiasi kikubwa, ambapo kuna mgawanyiko kati ya viongozi wa chama tawala cha Jubilee.

Upande mmoja ni wanaomuunga mkono Rais, na kwa upande mwingine ni wanaomfuata naibu wake, Dkt William Ruto.

Wote hulaumiana kwa kutatiza shughuli za serikali kwa kiwango cha kushindwa kutekeleza ahadi za maendeleo zilizotolewa kwa wananchi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita.

Habari zinazohusiana na hii

UHURU AMTULIZA RAILA

Wababaisha ‘Baba’

ODM: Raila anachezwa

Kingi amzima Raila

Kichwa kinauma

Raila akausha marafiki