Thirdway lawamani kuhusu kesi inayopinga BBI

IBRAHIM ORUKO na WALTER MENYA

MAWAKILI wa Chama cha Thirdway Alliance, wamelaumiwa kwa kukataa kuondoa kesi inayopinga marekebisho ya katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) licha ya chama hicho kutaka kesi iondolewe mahakamani.

Bw Paul Mwangi anayewakilisha kamati simamizi ya BBI, amewakashifu mawakili hao huku akishuku kuna watu wanaowasukuma waendelee mbele na kesi hiyo hata ikiwa chama kimeamua kuiondoa.

Kesi hiyo ilikuwa imewasilishwa na chama hicho kikitaka mswada wa marekebisho ya katiba usipelekwe kwa mabunge ya kaunti.

Chama hicho kiliamua kuondoa kesi ilipobainika kuwa mswada huo ulikuwa tayari ushafikia madiwani.

“Tumejijazia kuwa kuna mpinzani wa BBI ambaye maagizo yake ni makuu kuliko ya walalamishi waliotajwa katika kesi hii, aliyepanga njama nao kuhujumu mfumo wa haki,” Bw Mwangi aliandikia mawakili wa chama hicho katika mojawapo ya baruapepe zilizoonekana na Taifa Jumapili.

Kuna wasiwasi kuwa huenda Bw Elias Mutuma, ambaye ni wakili mkuu wa chama katika kesi hiyo, alishurutishwa kukataa maagizo ya kuondoa kesi hata ingawa awali alikuwa amekubali matakwa ya mteja wake.

Mnamo Januari, chama hicho kiliwasilisha ombi kwa Mahakama Kuu kikitaka maagizo ya kuamrisha Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) isiwasilishe mswada wa BBI kwa mabunge ya kaunti.

Ilipofika Februari 15, Kamati Simamizi ya chama hicho kwa mashauriano na wanachama ilifanya mkutano wa mtandao ambapo uamuzi ulipitishwa kuondoa kesi kwani ilipitwa na wakati. Chama hicho kiliwasilisha maagizo siku hiyo hiyo kwa kampuni ya mawakili ya Mutuma Gichuru Associates, ambayo ilithibitisha kupokea maagizo ya kuondoa kesi.

Habari zinazohusiana na hii

BBI YAINGIA ICU

Kwani kuliendaje?