• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
DINI: Usikate tamaa, kipenga cha mwisho bado

DINI: Usikate tamaa, kipenga cha mwisho bado

Na FAUSTIN KAMUGISHA

MAMBO hayajaisha mpaka Mungu aseme yameisha.

Mwisho hauji upesi.

Mungu ni refa katika mchezo wa maisha. Ameshika kipenga. Usikate tamaa, kipenga cha mwisho bado, filimbi ya mwisho bado.

Kuna mchungaji aliyeenda kutazama mashindano ya mpira kati ya timu mbili. Alikuta shabiki mmoja kijana anashangilia kwa nguvu, akipiga vuvuzela.

Mchungaji aliuliza, “Ngapi ngapi?” Kijana alijibu, “3-2.”

Mchungaji aliongeza maneno, “Inamaanisha timu yako inaongoza?”

Kijana alisema, “Hapana tumepigwa.” Mchungaji alizidi kuhoji, “Mbona unashangilia kwa nguvu?”

Kijana kwa matumaini alijibu, “Kipenga cha mwisho bado.”

Mwisho wa mechi matokeo yalikuwa 4-3. Timu yake ilibeba tawi la ushindi.

Mwizi upande wa kulia wa Yesu alitundikwa msalabani akiwa mwizi. Mwizi upande wa kulia kimapokeo anaitwa Dismas au Demacus.

Anaitwa Mwizi Mwema kwa sababu alitubu. Aliaga dunia akiwa Mt Dismas, aliiba mbingu dakika za lalasalama.

Sala yake ya mwisho ilikuwa, “Ee Yesu nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.” (Luka 23: 42).

Hii ilikuwa sala yake ya mwisho, la labda sala yake ya kwanza maishani. Alibisha hodi mara moja akafunguliwa.

Alitafuta akapata. Aliomba mara moja akapewa. Yesu alimwambia, “Amin, nakwambia, leo hivi utakuwa pamoja nami paradizoni.” (Luka 23: 43).

Jina Dismas maana yake hali ngumu. Ni jina la Kiebrania. Kwake hali ilikuwa ngumu ila baadaye ikabadilika. Magumu yakawa mepesi.

Wahaya wa Tanzania wana methali isemayo, “Ambaye hajaaga dunia usimgeuze kwa kijiti” (Atakafire otamuinduza kati).

Maskini hatabariki. Mjukuu wako anaweza kufanikiwa akakusaidia. Mtoto wako anaweza kufanikiwa akakusaidia. Bora uzima, lolote zuri linaweza kutokea.

Kuna methali nyingine isemayo, “Mungu alilokuwekea haliozi.”

Usikate tamaa kipenga cha mwisho bado.

Kuna mtu ambaye alikuwa kwenye mchakato wa kesi ya muda mrefu.

Hukumu ilikuwa inatolewa siku ya Jumatatu. Jumapili alienda kwenye zizi la ng’ombe na kujinyonga kwa kamba.

Jumatatu hakimu alitoa hukumu. Mtu huyo ushindi ulikuwa ni wake. Lakini alikwisha amejinyonga.

Alikata tamaa. “Hakuna mazingira ambayo hayana matumaini bali watu ambao hawana matumaini na mazingira hayo,” alisema William Barclay.

Usikate tamaa, kipenga cha mwisho bado. Kwenye kitabu chenye kichwa Never Give Up (Usikate tamaa kamwe), kuna picha ya ndege amemmeza chura.

Lakini chura amebana shingo ya ndege kichwa chake kisipite.

Kichwa cha chura kiko kwenye mdomo wa ndege. Bila shaka ndege alimtema chura. Ndege huyu alikuwa mfungwa wa matumaini.

Tuitwe wafungwa wa matumaini kama Zekaria asemavyo, “Enyi wafungwa wa matumaini.” (Zekaria 9:12).

Usipoteze mateso yako. Mwizi upande wa kushoto wa Yesu alipoteza mateso yake.

Alimtukana Yesu. Alimdhihaki Yesu. Kutukana ni kupoteza mateso yako. Kutukana ni kupoteza machozi yako. Kutukana ni kupoteza huzuni yako.

“Mmoja wa wale wahalifu waliotundikwa alimtukana akisema, “Je, wewe si Kristo? Basi, jiokoe mwenyewe na sisi pia.” (Luka 23: 39).

“Jeraha la maneno ni baya sana kuliko jeraha la panga.” (Ni methali ya kiarabu).

Ni kama mgonjwa anamtukana daktari. Anayetegemea kuzaa anamtukuna mkunga.

Usitukane wakunga na uzazi ungalipo. Cordell Hull alisema, “Usitukane kamwe mamba mpaka umevuka mto.”

Hata ukishavuka mto usitukane mamba. Ni kama mlipa kodi anatukana KRA.

Ni kama mtuhumiwa anamtukana hakimu. Ni kama mwanafunzi anamtukana mwalimu. Ni kama muuzaji anamtukana mnunuzi.

“Baadhi ya magoti yanapigwa pakiwepo na mzigo mzito moyoni; baadhi ya macho yanafunguliwa baada ya kichwa kuinamishwa,” alisema William Arthur Ward.

Macho ya Dismas Mwizi Mwema yalifunguliwa baada ya mateso.

Akiwa na mzigo mzito alisali akiomba akumbukwe katika ufalme wa Yesu.

You can share this post!

Amevutia Wakenya kwa kuongea Kiswahili sanifu

MALENGA WA WIKI: Kutana na Juma Mrisho ‘Ustadhi Chapuo’...