• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
JAMVI: Ushindi wa BBI rungu la kumtwanga Ruto

JAMVI: Ushindi wa BBI rungu la kumtwanga Ruto

Na BENSON MATHEKA

USHINDI mkubwa wa kupitishwa kwa mswada wa kubadilisha Katiba wa (BBI) na mabunge zaidi ya 40 ya kaunti, kumewatia nguvu vinara wa mchakato huo, Rais Uhuru Kenyatta, kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga na washirika wao kumpiga vita Naibu Rais William Ruto ambaye amekuwa akiupinga.

Hii inaweza kuwa pigo kwa azma ya Dkt Ruto ya kugombea urais ambayo amekuwa akiendeleza kupitia kampeni ya kusaidia maskini.

Wadadisi wa siasa wanasema kwamba kuidhinishwa kwa mswada huo na mabunge ya kaunti 43 yakiwemo ya kaunti za eneo la Rift Valley kunaweza kufifisha umaarufu wa Dkt Ruto nchini.

Tayari, vigogo wa kisiasa kutoka maeneo tofauti wameungana kupongeza mabunge ya kaunti kwa kupitisha mswada na kumuaibisha Dkt Ruto ambaye alikuwa ameapa kuuzima na kuzuia kura ya maamuzi kufanyika.

Mnamo Alhamisi, siku ambayo spika wa bunge Justin Muturi alitangaza kuwa amepokea ripoti kutoka kwa mabunge ya kaunti yaliyopitisha mswada huo, Rais Kenyatta, Bw Odinga, kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi wa chama cha Amani National Congress, Charity Ngilu wa chama cha Narc, Moses Wetangula wa Ford Kenya na Gidion Moi wa Kanu, walikutana katika kile kilichofasiriwa kuwa muungano mpya wa kuleta mabadiliko nchini.

“Tunapoanza hatua nyingine katika kuafikia marekebisho ya kwanza (ya Katiba ya 2010), tunatoa wito kwa Wakenya kutumia umoja wetu mpya na maafikiano makuu zaidi ya kisiasa kwa manufaa ya kudumu kwa taifa letu tunalolipenda. Mchakato wa BBI unawakilisha tukio nadra katika kizazi chochote na linalokomesha yaliyopita; ili kusuluhisha changamoto nyingi za kitaifa za muda mrefu ambazo zinatuzuia kuafikia Kenya yenye umoja na ufanisi kwa wote,” viongozi hao walisema kwenye taarifa ya pamoja.

Na katika hatua inayoonekana kutia nguvu mpya handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga iliyozaa mchakato wa sasa wa kubadilisha Katiba, vigogo hao saba walisema kwamba watatumia maadhimisho ya mwaka wa tatu wa handisheki hiyo mnamo Machi 9, 2021 kushauriana na wabunge na viongozi wa kaunti.

Wachanganuzi wa siasa wanasema ni wazi kwamba kuidhinishwa kwa mswada huo ni pigo kubwa kisiasa kwa Dkt Ruto ambaye amekuwa akipinga handisheki na BBI.

“Kupitishwa kwa mswada huo kunadidimiza nafasi ya Dkt Ruto kumrithi Rais Kenyatta kwa kupinga mradi wa kiongozi wa serikali ya Jubilee,” asema mchanganuzi wa siasa Patrick Siasi.

Anasema kwamba Dkt Ruto alijikaanga kwa kudharau vinara wa mchakato huo akijiona kuwa maarufu ilhali uliasisiwa na kuungwa na mkubwa wake.

“Kupitishwa kwa mswada huo na mabunge ya kaunti kunamaanisha kwamba Uhuru na Raila ndio wanasiasa maarufu zaidi mashinani na kupiga dafrau kampeni ya Dkt Ruto,” asema.

Mnamo Jumatano, Bw Odinga alimwambia Dkt Ruto kuwa asidhani Wakenya ni wajinga hata wanapomshangilia akiwapotosha kuhusu mchakato huo.

Kwa mujibu wa Profesa Nyaga Kindiki wa chuo kikuu cha Moi, kuidhinishwa kwa mswada huo na mabunge mengi ya kaunti kutaimarisha nafasi ya Bw Odinga kugombea urais.

Mhadhiri huyu pia anasema kwamba hatua ya mabunge kupitisha mswada huo ni ushindi mkubwa kwa Rais Kenyatta ambaye anataka kuacha kumbukumbu muhula wake wa pili uongozini utakapomalizika 2022.

Profesa Kindiki aliambia gazeti moja la humu nchini mapema wiki hii kwamba mswada huo ukipitishwa na bunge na kwenye referenda, Dkt Ruto anaweza kujipata katika upinzani.

Baadhi ya wachanganuzi wanasema kwamba kupitishwa kwa mswada huo na mabunge ya kaunti kutafufua juhudi za kumtimua Dkt Ruto ofisini na kuzima ndoto yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

“Walichojifunza vigogo wa kisiasa wanaomezea mate urais na ambao wanaunga mchakato huo ni kwamba, Dkt Ruto hana ushawishi mkubwa kwenye mabunge ya kaunti na pengine mashinani na ikiwa upo, umetikiswa. Hatua hii inaweza kufufua juhudi za kumuondoa ofisini,” asema Saisi.

Mnamo Alhamisi, Naibu Mwenyekiti wa chama cha Jubilee, David Murathe ambaye alikuwa wa kwanza kudai Dkt Ruto hatamrithi Rais Kenyatta alisema kwamba kuna mipango ya kumpokonya Dkt Ruto mamlaka yake.

Bw Saisi anasema kwamba ikizingatiwa kuwa hivi majuzi Rais Kenyatta alimtaka naibu wake kujiuzulu badala ya kukosoa serikali anayohudumia, si ajabu chama cha Jubilee kikaungana na washirika wake wapya kupata idadi ya wabunge kumuondoa Dkt Ruto ofisini na kumzima kabisa kushikilia wadhifa wa umma.

Mbunge wa Lugari Ayub Savula amekuwa akikusanya saini kutoka kwa wenzake kuunga mswada wa kumuondoa Dkt Ruto ofisini. Vigogo wa kisiasa ambao walikutana na Rais Kenyatta katika ikulu Alhamisi kushukuru mabunge ya kaunti kwa kupitisha BBI wamekuwa wakimtaka Dkt Ruto ajiuzulu.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kwamba vigogo wote wa kisiasa nchini wanaonekana kuwa upande wa serikali isipokuwa Dkt Ruto ambaye anacheza ngoma kivyake na kutengwa hata katika serikali aliyosaidia kubuni.

Hata hivyo, kuna wanaohisi kwamba Dkt Ruto si mwanasiasa wa kuzimwa haraka.

“Kwanza, kumuondoa ofisini si kazi rahisi na kuna athari zake ikizingatiwa kwamba ana wafuasi wengi. Pili, anaweza kutumia mabadiliko ya kikatiba kujijenga zaidi kwa sababu kutabuniwa nyadhifa anazoweza kutumia kurushia chambo wanasiasa wakuu wakiwemo wale wanaompiga vita kwa sasa. Hizi ni siasa na chochote kinawezekana,” aeleza mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.

Anaongeza kuwa Dkt Ruto amekuwa akitumia kila kombora la kisiasa analorushiwa kujijenga na hilo linawezekana hata kwa wakati huu ambapo anaonekana kulemewa.

You can share this post!

MALENGA WA WIKI: Kutana na Juma Mrisho ‘Ustadhi Chapuo’...

TAHARIRI: Siasa isituzuie kujali uchumi