TAHARIRI: Siasa isituzuie kujali uchumi

KITENGO CHA UHARIRI

SIASA zinapoendela kushika kasi nchini, ni muhimu kwa viongozi kutosahau majukumu wanayopaswa kutekeleza na kutofumbia macho changamoto zinazowakumba Wakenya.

Tangu 2020 tatizo kuu ambalo limekuwa likimwandama kila Mkenya ni ongezeko la gharama ya maisha. Hali hiyo ilichangiwa pakubwa na mchipuko wa janga la virusi vya corona.

Ingawa wengi walitarajia mwaka huu utakuwa wenye afueni, taswira ni ile ile.

Gharama za bidhaa za msingi kama mafuta na vyakula zinaendelea kupanda.

Majuma mawili yaliyopita, Mamlaka ya Kudhibiti Kawi (EPRA) iliongeza bei za mafuta kwa hadi Sh8, hatua ambayo iliwalazimu wafanyabiashara wengi kuongeza bei za bidhaa zao mara moja.

Tangazo hilo liliathiri kila sekta ya nchi. Wenye magari ya umma walilazimika kuongeza nauli, wakiwaacha wasafiri ambao hutumia magari hayo kwenda makazini mwao kila siku kwenye njiapanda.

Kutokana na mwelekeo huo, baadhi ya Wakenya wameripotiwa kuamua kutembea makazini mwao au hata kukwepa chakula cha mchana ili kupata nauli.

Kama hilo halitoshi, shule nyingi zilifunguliwa wakati wananchi wengi ambao ni wazazi walikuwa wakipitia masaibu hayo.

Hilo linamaanisha huo ni mzigo mwingine ambao waliongezwa, kwani lazima wagharamikie mahitaji ya kila siku ya wanao kama vile chakula na baadhi ya vifaa vya kimasomo wanavyoitishwa shuleni.

Chini ya mazingira kama hayo, ni vibaya kwa wanasiasa kuanza kuendeleza siasa kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI) na Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Ingawa masuala hayo mawili ni muhimu kwa nchi, wanasiasa hawapaswi kuyatilia mkazo kiasi cha kuwasahau wananchi.

Kile mwananchi anafaa kusikia kutoka kwa viongozi kwa sasa ni jinsi serikali itachukua hatua za haraka kumpunguzia mzigo mkubwa wa gharama ya maisha.

Ikizingatiwa serikali isharejesha viwango vya ushuru kama ilivyokuwa awali, utakuwa usaliti wa wazi ikiwa wanasiasa wataendelea kuyapuuza mahangaiko yanayowazonga wananchi.

Wito wetu kwa Rais Uhuru Kenyatta ni kuongoza harakati hizo, ili kuweka mfano utakaofuatwa na kuzingatiwa na wanasiasa wengine.

Hilo ndilo litawafungua macho kufahamu kuwa wao pia wana ndugu na jamaa wanaopitia katika hali kama hizo.

Habari zinazohusiana na hii