• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 11:28 AM
Mjane wa balozi wa Italia nchini DRC avunja kimya

Mjane wa balozi wa Italia nchini DRC avunja kimya

Na PATRICK ILUNGA

MWANDISHI WA NMG, Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)

WIKI moja baada ya kuuawa kwa Balozi wa Italia nchini DRC Luca Attanasio, mjane wake amevunja kimya chake kwa madai kuwa marehemu alisalitiwa.

Kwenye mahojiano na gazeti la Italia Corriere Della Sera, Zakia Seddiki alielezea jinsi mumewe alialikwa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Chakula Ulimwenguni (WFP) kukagua mradi mmoja unaotekelezwa katika shule moja karibu na mji wa Goma.

Bi Seddiki alishikilia kuwa shirika hilo halikuweka mikakati ya kiusalama kwa msafara wa balozi huyo.

“Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mume wangu kusafiri kutoka Kinshasa bila kusindikizwa na maafisa wa usalama wenye silaha. Lakini tulikuwa na imani na shirika hili la Umoja wa Mataifa,” akasema Bi Seddiki kwenye mahojiano.

“Hata hivyo, naamini kuwa Luca alisalitiwa na mtu fulani katika WFP ambaye alijua kuwa hawakuwa wamempa usalama wa kutosha,” akaongeza.

Balozi Luca aliuawa pamoja na watu wengine wawili waliokuwa katika ujumbe wake.

Mara baada ya msafara kushambuliwa Shirika la Mpango wa Chakula (WFP) la Umoja wa Mataifa (UN) lilituma salamu za pole kwa familia za wote walioangamia na vile vile kufikishja salamu hizo za pole kwa waliofanya kazi na wahanga na marafiki kwa jumla.

Waliofariki walikuwa ni balozi Luca, afisa katika ubalozi wa Italia na dereva wa WFP.

Picha ya zamani iliyotolewa Februari 22, 2021, Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Italia ikionyesha balozi wa Italia nchini DRC Luca Attanasio aliyeuawa kwenye shambulio mjini Goma. Picha/ AFP

Nadharia sawa na yake Bi Seddiki ilikuwa imetolewa na Nicaise Kibel Bel, mtaalamu wa masuala ya usalama na kijeshi ambaye anaishi Kivu Kaskazini.

Kulingana na Bel msafara wa balozi huyo ulipoanza safari, kulikuwa na watu fulani miongoni mwa ambao walitoa habari zilizowawezesha wavamizi kushambulio.

“Balozi huyo aliuawa kutokana na njama iliyopangwa vizuri na watu fulani,” akaeleza.

Lakini kulingana na Redio France International, inayopeperusha matangazo yake kwa lugha ya kifaransa, Naibu Mkurugenzi wa WFP nchini DRC Rocco Leone alipuuzilia mbali madai kwamba mauaji ya balozi yaliyotokana na utepetevu wa kiusalama.

Hata hivyo, Leone, ambaye ni miongoni mwa walionusurika katika shambulio hilo la Februari 22, 2021, alikataa kuzungumzia kwa kina kuhusu tukio hilo.

Kufuatia mauaji ya balozi Luca serikali ya DRC tayari imeanzisha uchunguzi kwa lengo la kuwatambua wahalifu.

Wakati huo huo, Italia imetaka “majibu ya haraka na kamilifu” kuelezea hali iliyosababisha kuuawa kwa balozi huyo.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

You can share this post!

Bayern Munich wanyanyasa Cologne na kuendeleza ubabe wao...

Polisi Kamukunji wachunguza kilichosababisha moto katika...