• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Visa vya uhalifu vyawatia hofu wakazi wa Thika

Visa vya uhalifu vyawatia hofu wakazi wa Thika

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Thika na wafanyabiashara wametaka maafisa wa usalama waingilie kati kwa kile walichotaja kama kuhangaishwa na vikundi vya wahalifu miongoni mwa vijana wa kurandaranda mjini (chokoraa).

Walisema vijana hao hutembea kwa vikundi vya vijana watano huku wakiwa wamejihami kwa visu.

Vijana hao hutekeleza uhalifu wao majira ya alfajiri na jioni watu wanaporejea nyumbani kutoka kazini.

Mnamo Jumamosi mwanamume mmoja aliyekuwa anatoka katika duka moja la jumla mjini Thika aliporwa bidhaa alizokuwa amenunua.

Kamanda wa polisi eneo la Thika Magharibi Bi Beatrice Kiraguri alisema tayari amepata ripoti kuhusu malamiko hayo na maafisa wa polisi wataendelea na msako.

Alisema watafanya juhudi kuwaondoa vijana hao mjini Thika ili wananchi waendeshe shughuli zao na amani.

Wafanyabiashara nao wanalalamika kuwa kila mara wakifungua sehemu zao za kufanyia biashara hupata zimevunjwa na wahuni hao.

Vijana hao inadaiwa hutisha yeyote anayekaiddi uhalifu wao huku wakimdunga kwa kisu.

Ilidaiwa wanavizia wapita njia vichochoroni na kando ya maduka madogo hasa yaliyoko katika kituo cha magari cha Thika.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Thika Bw Alfred Wanyoike alisema hatua kali inastahili kuchukuliwa dhidi ya wahuni hao kutoka na tabia zao.

“Hatutakubali mali ya watu kuibwa na wahuni ambao wanatamani vitu vya bure bila kuchoka,” alisema Bw Wanyoike.

Alitoa wito kwa maafisa wa usalama wafanye hima kuona ya kwamba hali ya usalama inaimarika mjini Thika.

Alisema ataandaa mkutano wa dharura na wafanyabiashara ili kujadiliana nao kuhusu hatua watakazochukua baadaye.

“Tayari nimefanya mkutano na kamanda wa polisi eneo la Thika Magharibi na amenijulisha maafisa wake wako mbioni kuwasaka wahalifu hao,” alisema Bw Wanyoike.

  • Tags

You can share this post!

Pigo kwa Barcelona fowadi Lautaro Martinez wa Inter Milan...

Leicester City kurefusha mkataba wa fowadi Harvey Barnes...