JAMVI: Joho na Kingi waanza kumkama Raila kijasho

Na MOHAMED AHMED

KINARA wa chama cha ODM Raila Odinga anaonekana kupitia wakati mgumu wa kisiasa katika ukanda wa Pwani ambapo chama chake kinaonekana kukosa mwelekeo.

Chama cha ODM kimeonekana kupigwa na mawimbi makali yanayotaka kukizamisha huku wandani wa Bw Odinga wakionekana kuwa mstari wa mbele kukiandama chama hicho.

Wakiongozwa na magavana Hassan Joho wa Mombasa na mwenzake wa Kilifi Amason Kingi, viongozi wa Pwani wameonekana kumpa Bw Odinga wakati mgumu ilhali kwa muda sasa amekuwa akifurahia ufuasi wao.

Bw Kingi amekuwa akisema kuna haja ya Pwani kujiondoa ODM huku naye Bw Joho akisema anataka kuungwa mkono na Bw Odinga chamani humo.

Katika mpango wake, Bw Kingi anataka kuviunganisha vyama vya Kadu Asili, Umoja Summit Party, Shirikisho Party of Kenya, Devolution Party of Kenya katika kuwa chombo kimoja ambacho anasema kitatumiwa na Wapwani kujiwakilisha.

Katika mahojiano, Bw Kingi amesisitiza kuwa kuna haja ya Pwani kuwa na chama mahsusi akitaja mifano ya viongozi wakuu waliounda muungano wa NASA akiwemo Kalonzo (Wiper) Musyoka, Musalia Mudavadi (ANC), Isaac Ruto (Chama cha Mashinani) na Moses Wetangula (Ford Kenya’s Moses) ambao alisema walikuwa na sauti ya kuwakilisha watu wao.

Bw Joho naye kwa takriban mwezi mmoja sasa amekuwa akisisitiza kuwa ni lazima Bw Odinga amuunge yeye mkono kwani kwa muda mrefu Pwani imemuunga mkono.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa za Pwani, wawili hawa wanatafuta mbinu ya kuwa na uwezo wa kusikika wakati nchi inapoelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Profesa Hassan Mwakimako ambaye ni mchanganuzi wa siasa asema kuwa hata hivyo, mwelekeo huu wa viongozi hawa unaonekana kumpa Bw Odinga wasiwasi kwa sababu wawili hawa ndio wamekuwa wakiendesha ajenda za Bw Odinga Pwani.

Anasema kwa sasa, sauti ya wakazi imekuwa ikisikika na mwito wao ni huo wa umoja ambao Bw Kingi na Joho wameshikilia na kuonekana kumtoa Bw Odinga kijasho.

“Bw Odinga amekuwa akifurahia ufuasi wa Pwani kupitia wakazi ambao wanampenda lakini sasa wakazi wanaoekana kubadilisha mwelekeo na ndiyo maana magavana hao wawili wameamua kumtangulia Bw Odinga,” akasema.

Alisema kuwa Bw Kingi na Bw Joho wanatumia mpango huo kuvutia wakazi hivyo basi huenda mpango huo ukamuumiza Bw Odinga iwapo hatachukua hatua za haraka.

“Ajenda zao zimeonekana kushika moto ijapokuwa inajulikana wanajipigania wao binafsi. Lakini kuna haja ya Bw Odinga kuchukua hatua za mapema la sivyo, ikikaribia 2022 basi wawili hao watakuwa wamepata nguvu zaidi,” akasema.

Aliongeza kuwa nguvu hizo huenda zikatumiwa kujitafutia matakwa yao kwa viongozi wengine akiwemo Naibu Rais William Ruto.

Dkt Ruto kwa upande wake pia ameonekana kumtatiza Bw Odinga kufuatia ziara zake za Pwani ambapo tayari ana ufuasi ijapokuwa ni mdogo sana kwa sasa.

Kufikia sasa, Dkt Ruto amenyakua viongozi kadhaa wa Kwale na wengine wachache kutoka kaunti ya Kilifi.

Baadhi ya viongozi ambao wanamuunga mkono Dkt Ruto ni wabunge Aisha Jumwa (Malindi), Owen Baya (Kilifi Kaskazini), Paul Katana (Kaloleni).

Wengine ni Gavana Salim Mvurya, mbunge wa Kinango Benjamin Tayari na mwenzake wa Lunga Lunga Khatib Mwashetani.

Inaaminika kuwa ni kufuatia matukio hayo ambayo yamemfanya Bw Odinga kupanga safari ya kuzuru ukanda wa Pwani wiki hii.

Bw Odinga anatarajiwa kuwepo Pwani kuanzia kesho (Jumatatu) hadi Alhamisi ambapo atahitimisha ziara yake kwa mkutano mkubwa katika Kaunti ya Mombasa.

Kiongozi huyo anarajiwa kuzuru kaunti za Taita Taveta na Kwale na kumalizia Mombasa.