• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
JAMVI: BBI yaacha Tangatanga Mlima Mkenya kwenye njiapanda 2022 ikinukia

JAMVI: BBI yaacha Tangatanga Mlima Mkenya kwenye njiapanda 2022 ikinukia

Na WANDERI KAMAU

HATUA ya mabunge ya kaunti katika ukanda wa Mlima Kenya kuupitisha mswada wa ripoti ya Mpango wa Maridhiano(BBI) wiki hii, imeuacha mrengo wa ‘Tangatanga’ katika ukanda huo kwenye njiapanda kisiasa.

Mabunge yote kumi katika kaunti za Nyeri, Nyandarua, Meru, Murang’a, Kiambu, Embu, Meru, Nakuru, Laikipia na Tharaka Nithi yaliupitisha mswada huo, licha ya kampeni kali ambazo zimekuwa zikiendeshwa na kundi pinzani dhidi ya ripoti hiyo.

Naibu Rais William Ruto pia amekuwa akisisitiza kwamba mswada huo haupaswi kupewa kipau mbele, kwani kuna masuala muhimu zaidi yanayowazonga Wakenya, kama vile hali mbaya ya uchumi wa nchi.

Baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakiendesha harakati za kuipinga ripoti hiyo Mlimani ni Seneta Irungu Kang’ata (Murang’a), wabunge Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Moses Kuria (Gatundu Kusini), Rigathi Gachagua (Mathira), Alice Wahome (Kandara), Ndindi Nyoro (Kiharu), Faith Gitau (Nyandarua) kati ya wengine.

Kwenye kampeni zake, kundi hili limekuwa likishikilia kuwa wenyeji wa ukanda huo hawahitaji BBI na badala yake wanataka kuelezwa kuhusu mikakati ambayo serikali ya Rais Uhuru Kenyatta itachukua kuimarisha sekta ya kilimo, ambayo ndiyo kitegauchumi kwa wengi wa wakazi.

Kwenye mahojiano, Bw Gachagua alisema matokeo hayo hayawatii wasiwasi hata kidogo, kwani uamuzi huo kamwe si “usemi wa wananchi.”

Bw Gachagua alisema kuwa madiwani wengi walipitisha ripoti hiyo baada ya “kuhongwa na serikali” kwa kupewa ruzuku ya Sh2 milioni kila mmoja kununua gari la kifahari.

“Hatuna wasiwasi hata kidogo, kwani mwananchi bado hajahusishwa kwenye mchakato huo. Ingawa kuna baadhi ya mapendekezo ambayo ni mazuri kwenye ripoti hiyo, msimamo wetu ni kuwa lazima sauti ya mwananchi isikike kikamilifu kabla ya maandalizi ya kura ya maamuzi,” akasema Bw Gachagua.

Wanasiasa hao wanasema ingawa wapinzani wao wanatarajia kwamba watamwacha Dkt Ruto baada ya matokeo hayo, hawatabadilisha msimamo wao.

Licha ya hakikisho hilo, imefichuka kuwa kuna madai kuhusu migawanyiko ambayo imeibuka katika kambi hiyo, inayohusu ushindani wa nani kati yao atakayeteuliwa na Dkt Ruto kuwa mgombea-mwenza wake 2022, ikiwa atawania urais.

Baadhi ya wanachama pia wameripotiwa kuanza kutathmini mielekeo yao kisiasa, hasa baada ya ripoti kuibuka kwamba Rais Kenyatta na viongozi wengine wa vyama vya kisiasa wameanza harakati za kubuni makundi yatakayoanza kampeni kali katika maeneo yao kupigia debe BBI.

Hayo yaliibuka baada ya mkutano uliofanyika Alhamisi kati ya Rais Kenyatta, kiongozi wa ODM Bw Raila Odinga, Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Seneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya), Seneta Gideon Moi (Kanu) na Gavana wa Kitui Charity Ngilu (Narc) katika Ikulu ya Nairobi.

Kwenye mkutano huo, iliripotiwa vigogo hao walikubaliana kubuni makundi ya viongozi na wataalamu watakaoanza kuwafikia na kuwafunza wananchi kuhusu yaliyomo kwenye ripoti hiyo kabla ya maandalizi ya kura ya maamuzi.

You can share this post!

JAMVI: Kusambaratika kwa NASA huenda itakuwa nafuu au...

JAMVI: Joho na Kingi waanza kumkama Raila kijasho