• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 PM
Bingwa mara mbili wa Safari Rally Hannu Mikkola afariki

Bingwa mara mbili wa Safari Rally Hannu Mikkola afariki

Na GEOFFREY ANENE

ULIMWENGU wa mbio za magari na michezo kwa jumla, unaomboleza kifo cha bingwa mara mbili wa Safari Rally, Hannu Mikkola.

Dereva huyo kutoka Finland, ambaye alishinda mbio hizo za kifahari za magari akiendesha Ford Escort RS 1600 mwaka 1972 na Audi 200 Quattro mwaka 1987, aliaga dunia Jumamosi akiwa na umri wa miaka 78.

Mwendazake Mikkola alizuru Kenya mara ya mwisho mwaka 2017 aliposhiriki marathon ya magari ya Kenya Airways East African Safari Classic Rally.

Miongoni mwa waliotuma rambirambi zao za pole kwa familia yake ni pamoja na dereva Charles Hinga na George Njoroge.

Afisa anayehusika na masuala ya udhamini kwenye Shirikisho la Mbio za Magari Kenya (KMSF) Sylvia King alisema pia ni huzuni kumpoteza Mikkola. “Mikkola alikuwa dereva wa kwanza wa kigeni kushinda Safari Rally mwaka 1972. Alikuwa mtu mtulivu. Mara ya mwisho nilikutana naye ilikuwa mwaka 2017 alipokuja Kenya kwa mashindano ya East Africa Classic Rally. Lala salama Hannu.”

Mikkola alizaliwa Mei 1942. Katika enzi yake kwenye mbio za magari, Mikkola aliwahi pia kutumia magari ya aina ya Volvo na Mazda. Alianza mashindano 123 ya mbio za magari za dunia (WRC) na kuendelea kushiriki mashindano ya mwaliko hadi 2017.

Bingwa wa zamani wa mbio za magari duniani Petter Solberg aliandika kwenye mtandao wa Facebook kuhuzunishwa kwake na kifo cha Mikkola, akimtaja kuwa shujaa.

You can share this post!

Shujaa, Lionesses wala rungu kali fainali ya Madrid Sevens

Arsenal waikomoa Leicester