• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
Msanii wa Rhumba awapa wakazi barakoa

Msanii wa Rhumba awapa wakazi barakoa

NA CHARLES ONGADI,

MTWAPA, KILIFI

SHUGHULI za kawaida zilisimama kwa muda mjini Mtwapa kaunti ya Kilifi baada ya mwanamuziki maarufu Petty Makambo wa nyimbo za rhumba kuwagawanyia wananchi barakoa.

Wanabodaboda na wachuuzi kandokando ya barabara ya Mtwapa kuelekea Kilifi mjini walisimamisha biashara zao kwa muda kupokea barakoa hizo .

“ Leo naadhimisha siku yangu ya kuzaliwa kiaina kwa kuwafaa wananchi wenzangu kwa barakoa kipindi hiki kigumu ambapo msambao wa virusi vya Corona umesimamisha shughuli nyingi duniani, “ akasema Makambo wakati wa mahojiano na Taifa Leo Digitali.

Kwa mujibu wa Makambo aliamua kutumia kiasi cha Sh50,000 aliyonuia kuwaandalia ndugu na marafiki sherehe murwa ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Petty Makambo akimpatia barakoa mfanyibiashara eneo la Mtwapa, Kilifi kujikinga dhidi ya virusi vya Corona. Mtwapa inafahamika kuwa na idadi kubwa ya watalii kutoka nchi za kigeni. PICHA/ CHARLES ONGADI

Makambo aliongeza kusema kwamba kuna baadhi ya wananchi ambao hawawezi kumudu kununua barakoa kila siku kutokana na hali mbaya ya uchumi kwa sasa.

Amewaomba wananchi daima kuzingatia sheria na masharti ya Wizara ya afya kuhusu maambukizi ya virusi vya Corona ili kufaulu kuuthibiti ugonjwa wa Covid-19.

Lucas Karisa ambaye ni mkazi wa Mtomondoni, Mtwapa, alimshukuru mwanamuziki huyu kwa hatua yake kuwajali wananchi wa kawaida kipindi hiki kigumu cha msambao wa virusi vya Corona.

Aliwaomba wahisani zaidi kujitokeza kuwasaidia wananchi kwa hali na mali kipindi hiki kigumu cha msambao wa virusi vya Corona.

Petty Makambo ambaye ni kiongozi wa bendi ya Beezy Academia aliandamana na kundi nzima ya bendi yake katika hafla hiyo fupi ya kuwagawanyia wananchi barakoa.

You can share this post!

Arsenal waikomoa Leicester

NDONDI: Kenya yasubiria nafasi mbili zaidi Olimpiki