• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
NDONDI: Kenya yasubiria nafasi mbili zaidi Olimpiki

NDONDI: Kenya yasubiria nafasi mbili zaidi Olimpiki

NA CHARLES ONGADI

LICHA ya kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) kufutilia mbali Mashindano ya Dunia kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki, bara lla Afrika lingali na afueni.

Mashindano ya dunia kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki yaliratibiwa kuandaliwa mwezi Machi jijini Paris nchini Ufaransa lakini yamefutiliwa mbali kutokana na msambao wa virusi vya Corona unaozidi kuongezeka nchini humo.

Kulingana na naibu mkufunzi wa timu ya taifa almaarufu ‘ Hit Squad’ David Munuhe, bara la Afrika limepewa nafasi 11 ya mabondia watakaochaguliwa kushiriki michezo hayo.

“ Sisi kama bara la Afrika ni afueni kwetu kupewa nafasi 11 tutakazopigania siyo kwa jukwaa bali kupitia kuchaguliwa mezani,” akasema Munuhe ambaye pia ni kati ya wakufunzi wa klabu ya ndondi ya Kenya Police maarufu kama ‘ Chafua Chafua’.

Kwa mujibu wa Kocha Munuhe, IOC itawachagua mabondia watakaoshiriki Michezo ya Olimpiki kulingana na viwango vyao.

Ameongeza kwamba huenda Kenya ikajiongezea nafasi mbili ama tatu katika idadi ya mabondia wawili ambao tayari wamefuzu kushiriki michezo hayo.

Timu ya taifa ya ndondi ‘ Hit Squad ‘ kabla ya kuyoyomea nchini Senegal kwa mashindano ya kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki mwaka jana. PICHA/ CHRALES ONGADI

Mabondia Nick ‘Commander’ Okoth anayezichapa katika uzito wa unyoya (feather) na mwanadada Christine Ongare katika uzito wa fly walifuzu katika mashindano ya kufuzu ya bara la Afrika yaliyoandaliwa mwezi Februari mwaka jana nchini Senegal.

Aidha, mabondia Elly Ajowi na Elizabeth Akinyi waliomaliza katika nafasi ya tatu katika mashindano ya kufuz ya bara la Afrika, wanapigiwa upatu kuchaguliwa katika nafasi 11 zilizopewa bara la Afrika.

Katika mashindano ya Senegal, Ajowi alipoteza pigano lake la uzito wa heavy katika hatua ya nusu fainali dhidi ya Youness Baallo kutoka Morocco huku Akinyi akinyukwa na Oumaya Bell Abbib wa Morocco katika uzani wa welter.

Kwa sasa timu ya taifa ‘ Hit Squad ‘ inaendelea na maandalizi makali katika ukumbi wa AV Fitness iliyoko mtaa wa Lavington jijini Nairobi chini ya mkufunzi mkuu Musa Benjamin anayesaidiana na John Waweru na Munuhe.

You can share this post!

Msanii wa Rhumba awapa wakazi barakoa

‘Red Devils’ wa zamani wanavyoisaidia Inter