• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:12 PM
Maelfu ya watahiniwa kukosa KCPE na KCSE

Maelfu ya watahiniwa kukosa KCPE na KCSE

Na WAANDISHI WETU

MAELFU ya watahiniwa wa mitihani ya darasa la nane (KCPE) na kidato cha nne (KCSE) hawako shuleni huku mitihani hiyo ikitarajiwa kuanza katika muda wa wiki tatu zijazo.

Walimu wakuu wameshindwa kuelezea waliko wanafunzi hao ambao hawakurudi shuleni Oktoba mwaka jana au Januari shule zilipofunguliwa kwa wanafunzi wa madarasa yote.

Hali hii inaibua wasiwasi kwamba idadi ya watahiniwa ambao huenda wakakosa kufanya mitihani mwaka huu, huenda ikawa ya juu kuliko miaka ya awali.Mitihani ya KCPE na KCSE itaanza mwezi huu huku ya kidato cha nne ikiendelea hadi mwezi ujao.

Familia nyingi zilihama maeneo zilizokuwa zikiishi baada ya kupoteza kazi na kukabiliwa na hali ngumu ya uchumi huku shule zikifungwa kufuatia athari za janga na corona.Maafisa wa elimu wameruhusu watahiniwa kubadilisha vituo vya kufanyia mitihani kukabiliana na mabadiliko hayo.

Uchunguzi wa Taifa Leo kote nchini ulifichua kwamba licha ya juhudi za wizara ya elimu na ile ya usalama wa ndani kuwasaka wanafunzi baada ya shule kufungwa wa muda mrefu kufuatia janga la corona, maelfu ya wanafunzi bado hawajarudi shuleni.Baadhi wameacha shule kabisa ingawa maafisa wa elimu hawataki kutoa idadi rasmi.

Taifa Leo imebaini kwamba wengi wa waliokosa kurudi shuleni waliolewa, wamejifungua au ni wajawazito.Nao wanafunzi wa kiume wameripotiwa kutafuta kazi ya vibarua wengi wao wakijiunga na biashara ya boda boda.Maafisa wa elimu walikataa kutoa idadi rasmi wakisema kwamba wameagizwa wasiongee na wanahabari.

Kaunti za eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa zinaonekana kuathiriwa zaidi ambapo wavulana ambao hawakurudi shuleni wanaendelea kupashwa tohara.Katika kaunti ndogo ya Baringo Kusini, watahiniwa 20 wa KCSE na idadi isiyojulikana ya watahiniwa wa KCPE bado hawajaripoti tangu shule zilipofunguliwa mwezi uliopita.

Ripoti ya idara za afya na elimu inaeleza kwamba wasichana 7, 600 walipata mimba shule zilipofungwa mwaka jana.Katika Kaunti ya Nandi, watahiniwa 193 wa KCPE waliopata mimba na 313 wa shule za sekondari hawakurudi shule.

Hata hivyo, Kamishna wa Kaunti hiyo, Bw Geoffrey Omoding, alisema mipango imefanywa kuwawezesha kufanya mitihani ya kitaifa.Katika Kaunti ya Samburu, wanafunzi zaidi ya 5,000 bado hawajarudi shuleni.

Hali hii imehusishwa na mimba za mapema, ukeketaji wa wasichana na wavulana kujiunga na marika wao wa Moran.Hata hivyo, mkurugenzi wa elimu wa kaunti hiyo, Bw David Koech, alisema bado hawajabaini idadi kamili ya watahiniwa ambao hawako shuleni.

Katika Kaunti ya Narok, ripoti zinasema wasichana 15,542 wa kati ya umri wa miaka 15 na 19 walipata mimba katika muda wa mwaka mmoja uliopita.

Na katika Kaunti ya Tana River, maafisa wa idara ya elimu wanawasaka watahiniwa watano walioacha shule kabla ya mitihani ya kitaifa huku Mandera wakitarajia kubaini idadi hiyo kufikia Machi 4.

You can share this post!

JAMAL MUSIALA: Usimuone alivyo kinda, ana thamani ya Sh3.2...

Maelfu waandamana kupinga ubaguzi katika utoaji wa chanjo...