• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:51 PM
Maelfu waandamana kupinga ubaguzi katika utoaji wa chanjo ya corona

Maelfu waandamana kupinga ubaguzi katika utoaji wa chanjo ya corona

Na AFP

MAELFU ya raia Jumamosi waliandamana katika miji kadha nchini Argentina kulaani sakata ya utoaji chanjo ya corona kwa mapendeleo kwa watu mashuhuri, iliyolazimisha Waziri wa Afya kujiuzlu.

Gines Gonzalez Garcia alijiondoa kazini wiki moja iliyopita kutokana na ombi la rais wa nchini hiyo baada ya kufichuka kuwa marafiki zake waliruka foleni ya kupata chanjo hiyo.

Waandamanaji waliobeba mabango yenye maandishi “Nipe chanjo yangu” na “Koma kutumia vibaya pesa zetu” walijikusanya nje ya makao makuu ya serikali katika jumba la Plaza de Mayo, jijini Buonos Aires.

“Walianza kutoa chanjo kwa marafiki zao serikalini. Hiyo sio vizuri. Wanahatarisha maisha ya wengine,” mwanandamanaji Irene Marcet aliambia shirika la habari la AFP.

Tangu Argentina ilipoanza kutoa chanjo kwa watu wake, ni wahudumu wa afya pekee ambao hadi Jumatano walikuwa wamekwisha kupewa chanjo hiyo. Ni siku hiyo ambapo watu wenye umri wa zaidi ya miaka 70 waliitwa wapewe chanjo hiyo ya kukinga dhidi ya maambukizi ya Covid-19.

Mnamo Jumatatu, serikali ilitoa orodha ya watu 70 ambao walipewa chanjo hiyo nje ya ratiba rasmi ya kampeni hiyo. Orodha hiyo ilijumuisha Waziri wa Fedha mwenye umri wa miaka 38 na rais wa zamani Eduardo Duhalde, mkewe na watoto wake.

Waandamanaji waliokuwa nje ya jumba hilo kwa jina Casa Rosada, ambalo lina afisi ya rais, walitundika kwenye jengo hilo mifuko ya kubeba maiti yenye majina ya viongozi watetezi wa serikali ambao walipewa chanjo.Rais Alberto Fernandez alilaani vitendo vya waandamanaji hao.

“Katika taifa la kidemokrasia, haifai kwa raia kuandamana kwa kutumia mifuko ya maiti yenye majina ya viongozi wa kisiasa nje ya jumba la Casa Rosada,” akasema kupitia mtandao wa Twitter.

“Huu ni ukiukaji wa uhuru wa kujieleza. Hatupasi kunyamazia vitendo vya kihuni kama hivi,” akaongeza.Hakuna kisa chochote kibaya kilitokea wakati wa maandamano hayo isipokuwa makabiliano madogo kati ya waandamanaji na viongozi wa kutetea haki za wafanyakazi karibu na makazi rasmi ya rais.

Maandamano mengine pia yalishuhudiwa katika miji kadhaa, ikiwemo Cordoba, Rosario na Mar del Plata.Argentina yenye jumla ya watu 44 milioni imenakili zaidi ya visa milioni mbili vya maambukizi ya Covid-19. Karibu watu 52, 000 pia wamefariki kutokana na ugonjwa huo hatari.

Kufikia Jumamosi, watu milioni moja walikuwa wamepewa chanjo, kulingana na ripoti kutoka Wizara ya Afya. Nchi hiyo imepokea dozi 1.22 milioni za chanjo kwa jina Sputnik V kutoka Urusi.

Kwingineko, Amerika Jumamosi iliidhinisha chanjo katoka kwa kampuni ya Johnson & Johnson kwa matumizi ya dharura kukabiliana na ugonjwa huo ambao umeangamiza zaidi ya Waamerika 500,000.

You can share this post!

Maelfu ya watahiniwa kukosa KCPE na KCSE

LEONARD ONYANGO: BBI ikipita mshahara wa wabunge ukatwe