• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Helikopta na magari ya kifahari viongozi wakimenyana wiki hii chaguzini

Helikopta na magari ya kifahari viongozi wakimenyana wiki hii chaguzini

Na WAANDISHI WETU

WANASIASA kutoka vyama mbalimbali wikendi waliongoza juhudi za kupigia debe wagombeaji wao katika chaguzi ndogo zinazotarajiwa kufanyika wiki hii.

Ikiwa ni wikendi ya mwisho ya kampeni kabla ya chaguzi hizo za Machi 4, wanasiasa walionyeshana ubabe kwa kutumia pesa nyingi, magari makubwa na helikopta mashinani.

Wengi wao walichangamsha eneo bunge la Matungu, Kaunti ya Kakamega na wadi ya Kiamokama, katika Kaunti ya Kisii.Jumla ya wagombeaji 15 wanang’ang’ania kiti cha eneo bunge la Matungu kilichosalia wazi kufuatia kifo cha marehemu Justus Murunga mnamo Novemba 15, mwaka jana.

Hata hivyo kivumbi kikali ni kati ya wagombeaji sita ambao ni pamoja na Peter Nabulindo wa chama cha Amani National Congress (ANC), David Were (ODM), Alex Lanya (United Democratic Alliance (UDA), Charles Kasamani (UDP), Auma Faida (Maendelea Chap Chap) na Paul Achayo (MDG).

Mnamo Jumamosi, kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, alizuru vijiji vya Mirere, Eshirumbwe na Itete kumpigia debe Bw Were ambaye ni mgombeaji wa chama hicho.

Bw Odinga alipaa kwa helikopta huku maafisa wengine wa ODM wakisafiri kwa magari ya kifahari kutoka kituo kimoja hadi kingine.Waziri huyo mkuu wa zamani aliandamana na Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya, mwenzake wa Vihiga Wilbur Ottichilo, aliyekuwa Mbunge wa Funyula, Bw Paul Otuoma, Mbunge wa Budalang’i, Bw Raphael Wanjala, Bw Geodfrey Osotsi (Mbunge Maalum) na Edwin Sifuna (Katibu Mkuu wa ODM).

Bw Odinga aliwasihi wakazi wa Matungu kumpigia kura mgombeaji wa ODM akimtaja kama kiongozi mwadilifu ambaye atayapa kipaumbele maslahi yao.

“Nimefanya kazi na Bw Were kwa muda mrefu na ninafahamu utendakazi wake. Hii ndio maana nimefika hapa binafsi kuwasihi mumpigie kura mnamo Machi 4,” akasema.

Mgombeaji wa ANC, Bw Nabulindo pia alipigwa jeki na mwanasiasa na mfanyabiashara wa Eldoret, Bw Bundotich Kiprop, maarufu kama Buzeki ambaye alimfanyia kampeni.

Mwanasiasa huyo ambaye alitua Matungu kwa helikopta aliandamana na Seneta wa Kakamega, Bw Cleophas Malala kumfanyia kampeni mgombeaji huyo wa ANC katika vituo vya Mirere, Mwananchi, Namamali Muslim na uwanja wa Matungu SDA.

Katika kaunti ya Kisii, viongozi wa mrengo wa Tangatanga wakiongozwa na Naibu Gavana Joash Maangi walitua katika wadi ya Kiamokama kumpigia debe mgombeaji wa chama cha UDA, Bw Moses Nyandusi Nyakeramba.

Wengine walioandamana naye ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Utekelekezaji wa Katiba (CIC), Bw Charles Nyachae, Kiongozi wa Chama cha Peoples Democratic Party (PDP) Omingo Magara na wabunge kadhaa wandani wa Naibu Rais William Ruto kutoka kaunti hiyo.

Duru zilisema kuwa Dkt Ruto amefadhili kampeni za Bw Nyakeramba kama hatua ya kwanza ya kuiwezesha UDA kukita mizizi katika Kaunti ya Kisii.

Kwingineko katika Kaunti ya Makueni jana, kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka na Gavana Kivutha Kibwana, walikita kambi katika wadi ya Kitise/Kithuki kupigia debe wawaniaji wa kiti cha udiwani kwa tiketi za vyama vya Wiper na Muungano, mtawalia.

Bw Musyoka alihutubia msururu wa mikutano ya hadhara kumfanyia kampeni mgombeaji wa Wiper Sebastian Muli huku Profesa Kibwana akifanya hivyo kurai wakazi wampigie kura mgombeaji wa chama cha Muungano Joseph Kioko mnamo Machi 4.

Ripoti za Shaban Makokha, Ruth Mbula na Pius Maundu

You can share this post!

WANTO WARUI: Likizo ya majuma 18 kwa wanafunzi wa gredi ya...

MARY WANGARI: Juhudi za pamoja zinahitajika kufanikisha...