• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
Chanjo ya corona kutua Nairobi Jumanne

Chanjo ya corona kutua Nairobi Jumanne

Na CHARLES WASONGA

HATIMAYE chanjo ya kudhibiti Covid-19 ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa hamu itawasili nchini mnamo Jumanne usiku, Machi 2.

Akiongea na wanahabari katika Kaunti ya Nyeri Jumapili, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alithibitisha kuwa kuna jumla ya vipimo (dozi) milioni 1.02 vya chanjo aina ya Astrazeneca kati ya vipimo milioni 4.1 ambavyo Kenya inatarajia kuagiza katika awamu ya kwanza.

Hatimaye Kenya inapanga kuagiza dozi milioni 24 za chanjo ifikapo Juni mwaka huu. Chanjo hiyo inaletwa nchini chini ya mpango wa usambazaji chanjo duniani kwa jina Covid-19 Vaccines Global Access (COVAX).

Waziri Kagwe alisema wahudumu wa afya katika kaunti zote 47 ndio watu wa kwanza ambao watapewa chanjo hiyo. Wengine ambao watanufaika kwa shehena hii ya kwanza ya chanjo ni maafisa wa usalama na walimu kote nchini.

“Wahudumu wa afya na wafanyakazi wengi walio mstari wa mbele katika vita dhidi ya corona kama vile walinda usalama na polisi watapata chanjo hiyo katika hospitali za rufaa katika ngazi za kaunti,” Bw Kagwe akaeleza.

Tangazo la Waziri huyo linajiri wakati ambapo viwango vya maambukizi ya corona na vifo vimeanza kupanda huku wataalamu wakionya kuwa huenda Kenya itashuhudia wimbi la tatu la maambukizi.

Mnamo Jumapili kwa mfano, kiwango cha maambukizi kilipanda hadi asilimia 9.9, kiwango cha juu zaidi katika kipindi cha miezi miwili iliyopita. Hii ni baada ya Kenya kuandikisha maambukizi mapya 329 baada ya sampuli kutoka kwa watu 3,282 kupimwa ndani ya muda wa 24.

Watalamu wanasema kuwa kiwango hichi cha maambukizi kinapanda kwa sababu watu wengine wamelegeza masharti ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Walio mstari wa mbele kuvunja masharti haya ya Wizara ya Afya ni wanasiasa ambao wanaendelea kuandaa mikutano mikubwa ya hadhara kote kupinga au kupigia debe mswada wa marekebisho ya Katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI).

Hii ndio maana Jumapili Waziri Kagwe aliwataka wananchini kuendelea kuzingatia kanuni za kudhibiti msambao wa corona licha ya kuwasili kwa chanjo.

“Ujio wa chanjo haumaanishi kuwa tumetelekeza masharti ya corona. Bado hatuko salama. Hii ni kwa sababu ulimwengu unakabiliwa na uhaba mkubwa wa chanjo wakati huu,” akaeleza Bw Kagwe.

Mwenyekiti wa Jopokazi la Ushauri kuhusu Chanjo ya Covid-19 Willis Akhwale alisema kuwa chanjo hiyo itapeanwa bila malipo katika hospitali za umma katika awamu hii ya kwanza.

Hata hivyo, katika awamu ya pili ya utoaji chanjo hiyo ambapo hospitali za kibinafsi zitahusishwa, vituo hivyo vya afya vitatoza ada ya Sh200 “kama ada ya usimamizi.”

“Kimsingi, chanjo hii itatolewa bila malipo katika hospitali za umma. Hii ni kwa sababu gharama yake imebebwa na serikali pamoja na wafadhili. Lakini katika awamu ya pili ambapo hospitali za umma zitahusishwa, ada kidogo ya usimamizi ya kima cha Sh200 itatozwa wananchi,” Dkt Akwale akasema Jumapili usiku kwenye mahojiano.

You can share this post!

Bitok ataja 20 Malkia Strikers ikijiandaa kuingia kambi ya...

RIZIKI: Mtangazaji wa redio asiyechagua kazi