• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Vijana walipanga kuvuruga hafla za Ruto – Polisi

Vijana walipanga kuvuruga hafla za Ruto – Polisi

Na MWANGI MUIRURI

MAAFISA wa usalama katika eneo la Kati walizima njama tano za kuzua fujo wakati wa ziara ya Naibu Rais William Ruto katika Kaunti ya Murang’a, Jumapili iliyopita.

Maafisa wa usalama waliozungumza na Taifa Leo kwa sharti kwamba majina yao yasifichuliwe, walieleza jinsi wanasiasa watano walidaiwa kupanga njama ya kuzua ghasia katika maeneo ya Gatura, Kirwara, Gatunyu, Kihumbuini na Ndakaini ambako Dkt Ruto alikuwa ametangaza kufanya mikutano.

Wanasiasa hao walianza kupanga ghasia wiki moja kabla ya ziara hiyo. Hafla kuu katika ziara ya Dkt Ruto ilikuwa hafla ya harambee katika kanisa la Gatura AIPCA na nyingine katika mji wa Gatunyu alikochangisha pesa za kusaidia chama cha waendeshaji boda boda cha Gatanga, na kisha kuhutubia mikutano ya hadhara.

Maafisa wa usalama walifichua kwamba kuanzia Ijumaa wiki jana, makachero walitumwa kufuatilia hali katika mitaa ya mabanda mjini Thika, ambayo wanasiasa hulipa vijana wanaowatumia kuzua fujo.“Mitaa tuliyopiga darubini ni Kiandutu, Kiang’ombe, Kiganjo, Gachagi na Makongeni.

Tulishika doria katika vituo vya magari ya uchukuzi ambayo huelekea Gatanga, hususan vilivyo mjini Thika na Njabini (katika kaunti za Kiambu na Nyandarua mtawalia) na kuzidisha doria zaidi barabarani.

“Pia tulipiga kambi katika masoko na kutangamana na watu, jambo ambalo lilituwezesha kuzima vitisho vyote ambavyo vilikuwa vimepangwa kutokea,” alisema afisa aliyehusika katika operesheni hiyo ya kuzuia fujo.

Polisi hawakutaka marudio ya kisa cha Septemba 4 ambapo vijana wawili kutoka mtaa wa mabanda wa Kiandutu waliuawa katika mji jirani wa Kenol, ambako makundi ya Kieleweke na Tangatanga yalikabiliana wakati Dkt Ruto akiongoza harambee katika kanisa la AIPCA eneo hilo.

Mjini Gatanga, ilifichuliwa kuwa maafisa wakuu wa polisi waliwapigia simu wanasiasa wawili wa eneo hilo ili kuwaonya wasihudhurie mikutano ya Dkt Ruto ambayo walikuwa wametangaza kuhudhuria.

“Wawili hao ni wa mrengo tofauti usiounga mkono Naibu Rais na walikuwa wametangaza kuwa wangehudhuria mikutano hiyo. Walikuwa wameandaa wafuasi wao kuandamana nao na kuwaagiza wakishambuliwa kwa maneno au kimwili, wawatetee,” Taifa Leo ilifahamishwa.

Mnamo Februari 12 alipohudhuria maadhimisho ya miaka 50 ya huduma ya upadri ya Askofu Mstaafu wa kanisa Katoliki Pater Kairo katika kanisa la Sacred Heart of Jesus Cathedral mjini Murang’a, Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i aliagiza maafisa wa usalama kukabiliana vikali na ghasia za kisiasa.

Mkuu wa polisi eneo la Gatanga, Bw Peter Muchemi, aliambia Taifa Leo kwamba “hatukutaka kubahatisha chochote. Kama wadumishaji usalama, tulihakikisha kila kitu kilikuwa sawa, na kwa usaidizi wa makamanda wetu wa kaunti tulifaulu kuzuia ghasia zozote,” alihoji.

Maafisa wa polisi kutoka Kandara, Maragua, Kigumo na Kahuro walitumwa Gatanga kusaidia wenzao kukabili changamoto zozote ibuka za kiusalama.Mkuu wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) eneo hilo, Bw John Kanda aliongeza: “Amani inapotishiwa huwa tunajihami na kuzima vitisho hivyo kwani nndio kazi yetu.”

Mnamo Ijumaa, afisa wa masuala ya habari na vijana katika mrengo wa Naibu Rais, Dennis Itumbi, alidokezea Taifa Leo kwamba baadhi ya wanasiasa wa Gatanga walikuwa wamepanga njama ya kupeleka wahalifu kuzua ghasia eneo hilo ili kupaka tope vuguvugu la kisiasa la Dkt Ruto, almaarufu hasla.

Alisema njama hiyo ilihusu kuzomea na kushambulia umma, wizi na kufanya Ruto kutofika vituo alivyopanga mikutano ili kumsawiri kama asiye maarufu na asiyependwa eneo hilo.

Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata aliunga madai hayo Jumamosi aliposema kwamba kulikuwa na njama ya kuua amani eneo la Gatanga kwa kuzua ghasia na akahimiza wapinzani wa Dkt Ruto kukumbatia siasa za ushawishi badala ya kutumia fujo.

Mmoja wa maafisa wakuu wa usalama alifurahi ziara ya Dkt Ruto ilipokamilika bila kisa cha ghasia akaandika katika mtandao wa kijamii: “Kwa mara nyingine, juhudi za pamoja za maafisa wa usalama kutoka kaunti yetu kuu ya Murang’a walidumisha usalama katika ziara ya Naibu Rais kaunti ya Murang’a. Kila tukio huwa ni funzo. Yaliyotokea katika ziara yake ya awali Septemba 4 ambayo watu wawili walikufa hayakupatiwa nafasi licha ya majaribio. Visa vyote vilizimwa vilikopangwa.”

Jana, Mshirikishi wa eneo la Kati Wilfred Nyagwanga alipongeza maafisa wake wa usalama kwa kusimama kidete, kuepuka siasa za mirengo na kutekeleza jukumu lao la kulinda maisha na mali.Bila kufafanua, Bw Nyagwanga alisema “ kulikuwa na majaribio ya kuvuruga amani kwa njia kubwa lakini nafurahi kwamba maafisa wangu waliweza kuyazima yalikoanzia.”

Bw Nyangwanga alisema kwamba maafisa wake wamejitolea kuhakikisha kwamba hafla zote za kisiasa zitakuwa salama mradi tu sheria izingatiwe.

“Tunataka wadau wote kutusaidia na kutambua kwamba tuko tayari kusaidia nchi kuwa na amani. Iwapo sote tutapenda amani na kuidumisha, hatutakuwa na shida. Lakini ni kweli tunajua kuna watu wachache wanaofurahia ghasia. Hao ni wateja wetu na tumejitolea kuwapata,” alisema na kuongeza kuwa “ vita dhidi ya maadui wa amani havitajali hadhi katika jamii.’

You can share this post!

Duale azimwa kuandaa mswada wa kuzima ngono mitandaoni

Taabani kwa kutisha kumuua Rais Kenyatta