• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:55 PM
TAHARIRI: Mswada wa Duale usipingwe ovyo

TAHARIRI: Mswada wa Duale usipingwe ovyo

NA MHARIRI

PENDEKEZO la Mbunge wa Garissa Mjini, Bw Aden Duale, kwamba kuwe na sheria itakayotoa adhabu kali kwa utengenezaji na usambazaji wa filamu za ngono nchini, linastahili kuungwa mkono.

Mswada ulioandaliwa na mbunge huyo tayari umeibua hisia mseto miongoni mwa wananchi.Kwa upande mmoja, kuna viongozi wa kijamii wakiwemo wale wa kidini ambao wamemuunga mkono.

Lakini kwa upande mwingine, kuna watumiaji wa mitandao ya kijamii ambao wengi wanampinga.Sababu nyingi zimetolewa na wanaopinga mswada huo, lakini lililojitokeza sana ni kwamba kuna mambo muhimu yanayofaa kuteka akili za viongozi kuliko masuala kuhusu filamu na picha za ngono.

Inafaa ieleweke kuwa mizizi ya matatizo mengi yanayokumba nchi hii iko katika upotovu wa maadili.Iwe ni ugaidi, ufisadi, mauaji ya kiholela miongoni mwa mengine, ukichunguza kwa kina kuna uwezekano mkubwa utakuta mengi husababishwa na uozo wa maadili katika jamii.

Hivyo basi, hata tunapopambana na maovu haya yanayotusababishia hasara kila kukicha, si makosa kama wengine wetu watatafuta njia za kurekebisha maadili kitaifa.

Si siri kwamba uozo wa kimaadili umekithiri mno miongoni mwa wananchi, wakubwa kwa wadogo katika enzi hizi ambazo karibu kila binadamu amekumbatia tekinolojia za habari na mawasiliano kimitandao.

Tunafahamu kuwa hata mswada wa Bw Duale ukipita uwe sheria, bado kutakuwa na changamoto kwani kwa kawaida ni vigumu kurekebisha tabia za halaiki ya watu kupitia kwa sheria.

Hata hivyo, kama sheria hii itasaidia kuzuia watu kutumia uhuru wao wa kupeperusha habari kuleta uozo katika jamii, ni heri kuliko kuendelea kuishi kama kwamba hatuna uwezo wa kuchukua hatua yoyote ile.

Imekuwa kawaida ya Wakenya kukashifu hatua zozote zinazochukuliwa wakitumia hisia zao badala ya kuwaza kwa mapana. Itakuwa vyema kama wananchi watakuwa na tabia ya kutoa maoni kuhusu jinsi mapendekezo yanaweza kuboreshwa kwa manufaa ya kila mmoja, badala ya kuwa wepesi wa kupinga kila jambo.

Hiyo ni njia mojawapo ambayo inaweza kutusaidia kuboresha sera na sheria zetu kwa pamoja tukiwa na lengo moja la kuboresha taifa letu.

You can share this post!

Wamaasai wanavyovumisha utalii kupitia sherehe za Moran

Video za ngono zihalalishwe mitandaoni – AKS