Shehena ya chanjo ya corona yafika Kenya

Na CHARLES WASONGA

HATIMAYE shehena ya kwanza ya chanjo ya Covid-19 iliwasili nchini Kenya Jumanne usiku na kupokewa na maafisa wakuu wa serikali wakiongozwa na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe.

Chanjo hiyo aina ya AstraZeneca na iliyotengezwa katika Chuo Kikuu chs Oxford, Uingereza, ilisafirishwa nchini kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Hazina ya Elimu ya Watoto (UNICEF) chini ya mpango wa usambaza wa chanjo kwa mataifa masikini duniani, COVAX.

Wengine waliokuwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi kupokea shehena ya chanjo hizo iliyosafirishwa kwa ndege ya Shirika la Ndege la Qatar aina ya QR1341, ni mwakilishi wa Unicef nchini Maniza Zaman na mwakilishi wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) Dkt Rudi Eggers.

Hii ni siku ya kihistoria kwa Kenya na inaashiria hatua muhimu katika mchakato wetu wa kupambana na Covid-19. Tumekuwa tukitumia risasi za mipira katika vita dhidi ya janga hili lakini sasa tumepokea silaha hatari kama “machine gun” kupambana na janga hili,” Bw Kagwe ambaye aliandamana na mwenzake, Waziri wa Uchukuzi James Macharia akawaambia wanahabari.

“Hatua hii imewezeshwa na uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta na kazi nzuri ya Wizara ya Afya. Lakini muhimu zaidi ningependa kushukuru UNICEF,WHO na shirika la kimataifa la usambazaji chanjo ya corona (GAVI) kwa kufadhili usafirishaji wa chanjo hizi,” akasema Bw Kagwe.

Kenya ilipokea vipimo/dozi 1.02 milioni za chanjo hiyo ambayo ni sehemu ya dozi 4.1 milioni ambazo zinatarajiwa kuwasilishwa nchini kati ya mwezi huu na Juni, kusambazwa chini ya awamu ya kwanza ya utoaji chanjo.

Kando na UNICEF na mashirika mengine yaliyofadhili ununuzi na uwasilishaji chanjo hizo Kenya, Bw Kagwe alisema Ujerumani pia imeahidi Kenya msaada ya Sh198 bilioni kwa ajili ya kuiwezesha kupata chanjo zaidi.

Baada ya kuwasili chanjo hizo zilipelekwa kwa ghala maalum katika eneo la Kitengela, kaunti ya Kajiado.

Wizara ya Afya ilisema kuwa kutoka hapo, chanjo hizo zitasambazwa katika maghala tisa katika maeneo mbalimbali nchini ambako zitatolewa na kusambazwa katika hospitali za ngazi ya kaunti na kaunti ndogo.

Kando na chanjo UNICEF pia imeipa Kenya sindano 1,025,000 na masuduku 10,250 yenye mahitaji mengine ya utoaji chanjo.

Wiziri Kagwe alikariri kuwa wale ambao watapewa chanjo hiyo kwanza ni zaidi ya wahudumu wa afya 4,500 katika kaunti zote 47, walinda usalama na walimu ambao ndio wako katika hatari ya kuambukizwa corona kutoka na hali ya kazi zao.

Habari zinazohusiana na hii