• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Udikteta ulivyolemaza vita dhidi ya corona Tanzania

Udikteta ulivyolemaza vita dhidi ya corona Tanzania

Na MWANDISHI WETU

Mwezi Februari nilisafiri kutoka Uropa hadi Dar es Salaam, Tanzania. Ilikuwa ni safari ya kikazi ambayo pia nilijifunza tofauti kubwa iliyopo baina ya nchi ya Tanzania na nchi nyingine katika kujilinda, kuwalinda wengine na kuchukua tahadhari kipindi hiki cha ugonjwa wa corona.

Idadi kubwa ya wasafiri katika ndege niliyoabiri walikuwa ni watalii walioshuka Zanzibar kabla ya safari kuhitimishwa Dar es Salaam.Wasafiri wote tuliosafiri kwenye ndege ile tulikuwa tumevaa barakoa katika muda wote wa safari, na usafi ulikuwa wa hali ya juu, tukisafisha mikono kwa maji tiririka ama sanitaiza.

Hali ilikuwa tofauti baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, kwani wafanyakazi wengi wa uwanja wa ndege hawakuwa wamevaa barakoa na walikuwa wanaendelea na maisha kama vile hakuna ugonjwa wa corona.

Karibu Tanzania, ambako hadi kufikia mwanzoni mwa mwaka huu Rais John Pombe Magufuli alitangaza kwamba ugonjwa wa corona umetokomea nchini baada ya maombi na hivyo tuendelee kuishi maisha yetu kama kawaida.Mara ya mwisho Tanzania ilitoa takwimu za ugonjwa huu mnamo Aprili 2020 kukiwa na idadi ya wagonjwa 509 na vifo 21.

Baada ya hapo takwimu zikapigwa kufuli. Kabla la tangazo la kwamba corona imeisha nchini, jitihada za kujikinga zilikuwa zinaonekana kwa wananchi kuosha mikono mara kwa mara, matangazo ya redioni na maeneo mengine kuwahimiza wananchi kujilinda na hata kupunguza misongamano katika matatu na usafiri mwingine wa umma.

Baadaye ilitangazwa kwamba tunywe mchanganyiko wa chai ya tangaziwi na ndimu mara kwa mara na kujifukiza na majani mbalimbali ambayo kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Dkt Dorothy Gwajima, husaidia kupambana ama kuzuia na maambukizi ya corona.

Angalau kulionekana jitihada za kujilinda kwa muda wa miezi miwili, hadi mwanzoni wa mwezi Mei mwaka jana wakati Rais Magufuli alipotangaza corona imeisha Tanzania.

Watu wakajiachia, barakoa wakatupa kule, misongamano katika matatu ikarudi kama awali na hata kuosha mikono hakukutiliwa maanani tena. Tangu hapo kauli ya Watanzania ikawa kwamba corona haipo tena Tanzania.

Wakati nchi nyingine duniani zikiimarisha hatua za kukabiliana na ugonjwa huu, Tanzania ikawa ni “kitovu cha utalii”. Ikawa ukifika katika mji wa Dar unakuwa na uhakika wa kuburudika kwenye mabaa hadi asubuhi, kwenda kushuhudia mechi ya mpira uwanjani na kutembea popote utakapo kwa muda wowote utakao.

Jambo ambalo lilinishangaza ni idadi kubwa ya wageni niliokutana nao sehemu mbalimbali wakiwa hawajavaa barakoa na wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.

Kwa mujibu wa daktari mmoja wa hospitali ya kibinafsi jijini Dar es Salaam, awamu ya kwanza ya corona nchini Tanzania, wananchi walitengeneza kinga ya jumla (herd immunity), ambayo huenda ilisaidia idadi kubwa ya watu kuugua na kupona na kutokuwa na idadi kubwa ya vifo.

“Watu hawakufungiwa ndani, hivyo walikuwa wakiambukizana bila kufahamu ni wagonjwa. Waliokuwa na kinga ndogo waliugua na huenda walikufa, na wale waliokuwa na kinga imara waliugua na kupona. Hivyo yawezekana wengi tuliugua, kwani hatukuwa tunapima. Mtu anaweza kuwa anajisikia homa kiasi, anakunywa tangawizi na dawa ya maumivu na baada ya siku chache anajisikia amepona,”akafafanua daktari huyo.

Hali ilivyo sasa

Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, kumekuwa na taarifa za watu kupoteza maisha sababu ya kile ambacho kimekuwa kikiripotiwa kama “matatizo ya kupumua.”

Ama kwa kitaalamu “acute pneumonia.”Daktari mmoja wa Hospitali moja kibinafsi Dar es Salaam, niliyepata nafasi ya kuzungumza naye akitaka jina lake libanwe kwa kuhofia usalama wake, anasema katika hospitali za binafsi idadi ya wagonjwa wenye dalili za corona imeongezeka maradufu.

“Hadi kufikia Desemba tulikuwa tunapokea wagonjwa wasiozidi 10 kwa wiki. Lakini hivi sasa idadi hiyo imeongezeka mara nne,” akaeleza.Kwa mujibu wa daktari huyo, wahudumu wa afya wamepigwa marufuku kuwaambia wagonjwa kuwa wanaugua corona na badala yake wameagizwa waripoti maradhi hayo kama “acute pneumonia.”

“Tunajua wagonjwa wanaugua corona, lakini tunashindwa kutoa taarifa halisi kwao,” akaeleza daktari huyo.Mnamo Alhamisi iliyopita, Mbunge wa Mbulu, Zacharia Isaay alizungumza bungeni kwamba amekuwa akifufuliza kuhudhuria mazishi ya wananchi wa eneo bunge lake ambao wote wanakufa kwa nyumonia.

“Serikali iache kigugumizi kuhusu suala hili wakati watu wanakufa katika eneo bunge langu. Nimechoka kuhudhuria mazishi, hata leo wanamzika mtoto wa diwani mmoja,” akasema Isaay ambaye ni mbunge wa chama tawala cha CCM.Akaongeza: “Hata jana nilienda hospital ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma kwa ajili ya vipimo binafsi na nikaambiwa mitungi yote ya oksijeni inatumika.”

Watu wengi wanaumwa. Sasa nimeamua kuzungumza hili wazi, kama kuna mtu atakwazika, ni shauri yake, mimi nimezungumza.”Kanisa Katoliki lan Tanzania pia limetoa taarifa rasmi ya kuwatahadharisha waumini wake wachukue tahadhari ya kujilinda na corona.

Katika hatua nyingine ambayo pia imekuwa inazungumziwa kwa minong’ono mitaani, ni pale Rais Magufuli alipotangaza kwamba Tanzania haitahitaji chanjo dhidi ya virusi vya corona.

“Kama wao wanajua kutengeneza chanjo kwa nini hadi sasa hawajaleta chanjo ya malaria ama kansa? Akasema Rais Magufuli katika mkutano mmoja wa hadhara.Matokeo yake, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeiondoa Tanzania miongoni mwa nchi ambazo zinatarajiwa kupatiwa chanjo ya virusi vya ugonjwa huo kuanzia mwaka huu.

Habari za corona kubanwa

Tatizo lingine ni kuwa Watanzania hawako huru kuzungumzia suala la corona, na habari nyingi zinatolewa na kupatikana katika mitandao ya jamii ikiwemo Twitter na Instagram.

Hata nilipojaribu kupata maoni, wengi wa aliotaka kuhoji walikataa kuzungumza wakihofia usalama wao. Hivi sasa viongozi na wataalamu wetu wa afya wamejikita katika kuhimiza upigaji nyungu (kujifukiza), na matumizi ya dawa asilia.

Lakini je, hizi dawa zinatibu kweli? Bila shaka mtu yeyote mwenye akili timamu atatambua kuwa kinachoendelea ni utaratibu wa kuwaondolea hofu Watanzania, kwa njia mbadala na maneno ya faraja.

Lakini je, nchi inafanya nini kumuokoa Mtanzania?Ni dhahiri kuwa kuna tatizo kubwa katika serikali ya Tanzania katika kushughulikia ugonjwa huu kuliko wengi tunavyojua.Watanzania wana kila sababu ya kuwahoji viongozi ili waseme ukweli.

Waseme ni kitu gani kinachowazuia kwenda sambamba na jumuia ya kimataifa, pamoja na shirika la WHO katika kupambana na ugonjwa huu. Ni hatua gani wanachukua katika kuboresha matibabu ya corona katika hospitali nchini na kwa kutumia taaluma ya kisasa badala ya mitishamba.

You can share this post!

BBI kuwasilishwa bungeni kesho

Ruto aonywa asifuate nyayo za Raila kisiasa