• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Mkuu wa hospitali aamriwa amfikishe Sonko kortini

Mkuu wa hospitali aamriwa amfikishe Sonko kortini

RICHARD MUNGUTI na WINNIE ATIENO

KINARA wa Nairobi Hospital na afisa anayesimamia masuala ya kesi katika tume ya kupambana na ufisadi nchini (EACC) Jumanne waliamriwa wamfikishe kortini aliyekuwa Gavana wa Nairobi Bw Mike Sonko kujibu kesi ya ufisadi wa Sh14milioni.

Akitoa maagizo hayo , hakimu mwandamizi mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bw Peter Ooko aliwataka maafisa hao wamfikishe kortini Bw Sonko saa tatu mnamo Machi 4, 2021.

Bw Ooko alitoa agizo hilo baada ya malumbano makali kati ya mawakili wa Sonko na viongozi wa mashtaka.

Mawakili wa Sonko Dkt John Khaminwa na Wilfred Nyamu walitaka kesi ya Sonko iahirishwe kwa muda wa miezi miwili lakini viongozi wa mashtaka wakasimama kidete na kuomba korti ishurutishe Nairobi Hospital na afisa wa EACC wamfikishe kortini gavana huyo anayekumbwa na kashfa za ufisadi Machi 3.

Lakini ombi hilo la viongozi wa mashtaka lilikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Dkt Khaminwa , Bw Nyamu na wakili Paula Atukunda waliosema “afya ya kila mmoja ni muhimu.”

“Sio kupenda kwa Bw Sonko alazwe hospitali. Aliugua na hapasi kukimbizwa kortini kuendelea na kesi kama sio buheri wa afya,” akasema Dkt Khaminwa huku akichemka kwa hasira.

Akaendelea kusema ,”Ikiwa hii mahakama inataka kuendelea na kesi dhidi ya Sonko, basi iahirishe vikao vya hii kesi na kuvipeleka hospitalini anakolazwa Sonko.”

Wakili huyo mkongwe mwenye tajriba ya juu katika masuala ya sheria na aliye na umri wa miaka 85 alilalama kortini akisema, “Katiba ya nchi hii ambayo ndiyo sheria kuu inasema kila mmoja lazima awe na afya njema ndipo ashiriki katika midahala na ujenzi wa afya.Je mmoja ataendelea aje kusikiza kesi na kujibu mashtaka akiwa anaugua na mwenye maumivu makali?”

Wakili huyo aliwakashfu viongozi wa mashtaka kwa msimamo wao na hari ya kumtaka Bw Sonko afikishwe kortini ilhali anaugua.

Mahakama iliombwa isiwe na haraka ya kumfikisha Sonko kortini akiwa mgonjwa.

“Nataka kuikumbusha hii mahakama kwamba aliyekuwa afisa mkuu serikali Bw Gakuo alifariki akiwa gerezani kwa sababu ya msimamo wa afisa ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma.Hatutaki Sonko aathirike kiafya kwasababu ya msimamo huu mkali wa Serikali,”Dkt Khaminwa.

Wakili mwenzake Bw Nyamu alieleza korti kuwa Bw Sonko anahitaji kusafiri hadi Afrika kusini kwa matibabu maalum.

Wakili huyo alitofautiana vikali na viongozi wa mashtaka waliosisitiza lazima Bw Sonko afike kortini.

Walimsihi hakimu aagize Sonko afikishwe kortini Machi 3 2021 lakini Nyamu akasema “ watakuwa mahakama ya Kahawa ambapo idara ya polisi wa kupambana na ugaidi (ATPU) wamewasilisha ombi gavana huyo anayekumbwa na utata mwingi azuiliwe kwa siku 30 kuhojiwa kuhusu ushirikiano na ufadhili wa ugaidi nchini.

ATPU imedai Sonko amekuwa akifadhili wanamgambo kuzua fujo nchini madai ambayo Sonko ameyakana kata katu.

Sonko amesema ametumbukizwa katika lindi la kesi sisizo na mbele wala nyuma kwa sababu ya msimamo wake kisiasa.

Mahakama ilikabidhiwa ripoti ya uchunguzi aliofanyiwa Sonko Februari 19,2021 na wataalam wanne wa matibabu katika hospitali kuu ya Kenyatta (KNH).

Mawakili Khaminwa na Nyamu walipinga ripoti hiyo ikisomwa na kutegemewa katika utoaji wa mwelekeo ikiwa Sonko atafika kortini au la.

Akasema Bw Nyamu,“Hii ripoti ni ya kisiri kuhusu afya ya Sonko.Haipasi kutangazwa kamwe adharani.Ripoti hii iliitishwa na hakimu mkuu Douglas Ogoti na wala sio Bw Ooko.Afisa za DPP na EACC zimekosa kuwasilisha ripoti hii na hatuna nakala yake ikitiliwa maanani ni ya mteja wetu.”

Bw Nyamu alisema hata mawakili wa washukiwa wengine wawili walioshtakiwa pamoja na Sonko hawapasi kupata nakala ya ripoti hiyo.

Baada ya cheche za maneno na kulumbano vikali , Dkt Khaminwa aliomba vikao vya adharani viahirishwe kisha waende katika afisa ya Bw Ooko wamweleza jambo faraghani.

Mawakili wa Sonko Dkt John Khaminwa (kulia) na Wilfred Nyamu wakisubiri kortini. PICHA/ RICHARD MUNGUTI

Vikao viliahirishwa kisha mawakili wote wakaenda afisini kwa Bw Ooko. Baada ya muda walirudi kortini na wote walinyamaza na kutulia vitini tulii huku wakisubiri hakimu atoe uamuzi kuhusu ombi la kesi kuahirishwa kwa miezi miwili.

Akitoa uamuzi ,Bw Ooko alisema amesoma na kukagua ripoti za madaktari na “ hajaona popote katika taarifa za hospitali kwamba Sonko hawezi kusimama ama hawezi kuelewa ushahidi kesi ikiendelea.”

Hakimu aliagiza Sonko afikishwe kortini Machi 4 kwa vile Machi 3 atapelekwa katika mahakama ya Kahawa kuhusiana na kesi ya ugaidi.

Sonko amekanusha kesi hiyo ya ufisadi wa Sh14milioni.

Sonko yuko kwa dhamana.

Mbali na kesi hii Bw Sonko anakabiliwa na kesi nyingine mbili zinazohusishwa ufujaji wa zaidi ya Sh354milioni.

Mnamo Alhamisi Bw Sonko atafikishwa mbele ya hakimu mkuu Douglas Ogoti anayesikiza kesi nyingine ya upokea hongo dhidi ya gavana huyu wa zamani mbishi ya Sh10milioni.

Katika kesi hiyo Bw Sonko ameomba hakimu ajiondoe kuisikiza kwa vile “ atamwonea na haki haitatendeka.”

  • Tags

You can share this post!

Diwani ang’olewa uongozini kutokana na hongo

Azuiliwa kwa kumuua nduguye wakipigania mwanamke