• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Azuiliwa kwa kumuua nduguye wakipigania mwanamke

Azuiliwa kwa kumuua nduguye wakipigania mwanamke

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA wa upelelezi wameruhusiwa na mahakama kumzuia korokoroni mwanaume aliyemuua nduguye wakipigania mwanamke.

Mshukiwa huyo wa mauaji Hussein Chemwor Maina atakaa rumande kwa siku 14 huku polisi wakimhoji kuhusiana na mauaji ya kinyama ya Noah Kibiama Maina mnamo Februari 24, 2021 katika mtaa wa Kayole, kaunti ya Nairobi, wenye visa vingi vya uhalifu.

Hakimu mkuu Bw Angelo Kithinji, alifahamishwa na Inspekta Moses Kenga kwamba ripoti ililiwasilishwa kwa maafisa wa uchunguzi wa jinai katika kituo cha polisi cha Kayole kuwa Chemwor alimwinukia nduguye na kumuangamiza baada ya mzozo kuhusu kidosho.

Insp Kenga alieleza korti kuwa , polisi wanamhoji Chemwor huku wakilenga kumfungulia shtaka la mauaji kinyume cha sheria nambari 203 na 204.

Alisema polisi wanahitaji muda kufanyia maiti upasuaji kubaini kiini cha kifo chake. “Polisi wanahitaji kumpeleka mshukiwa kupimwa akili kubaini ikiwa ubongo wake ni timamu,” hakimu alielezwa.

Pia korti ilijuzwa, polisi watawasaka mashahidi walioshuhudia kisa hicho waandikishe taarifa ndipo iambatanishwe pamoja kabla ya kuwasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji kutoa ushauri kabla ya shtaka la mauaji kusajiliwa.

Chemwor anadaiwa alimuua nduguye Noah Kibiama Maina kwa kumchoma kisu upande wa kulia wa kifua chake na vile vile alimdunga shingoni walipotofautiana kuhusu msichana mrembo mithili ya Malaika mkazi wa eneo la Soweto mtaani Kayole mashariki mwa jiji la Nairobi.

Duru zasema Chemwor alikuwa anammezea mate Bi Kisura huyo ambaye alikuwa ameyeyushwa moyo na marehemu.

Uchunguzi wa muda uliofanywa umebaini , Chemwor hakuwa na misitari ya kumridhisha mwanadada huyo na kamba zake za maneno hazikuweza kumfunga msichana huyo wa watu kwake.

Polisi wamesema Chemwor aliamua kuyachukua maisha ya nduguye ndipo awachwe akitamalaki katika ulingo huo wa mapenzi.

Siku hiyo ya Feburuari 24 ndiyo Chemwor aliingiwa na shari kisha akajihami kwa kisu na kuingia chumbani mwa nduguye na kumdunga hadi mautini.

Kibiama hakutazamia nduguye Chemwor alikuwa amemwazia mabaya. Kabla ya kupambanua kilichokuwa kikijiri tayari kisu kilikuwa kimezama shingoni na ukulele alioutoa haungewavuta majirani kumwokoa.

Rabsha iliyosikika chumbani ilikuwa hafifu. Aliaga akipelekwa hospitali ya Mama Lucy Kibaki iliyoko mtaa wa Umoja III Nairobi.

Baada ya kuyatwaa maisha ya nduguye Chemwor alizama katika mtaa huo na kujificha akiukwepa mkono wa sheria.

Lakini kama vile wahenga walisema mbio za sakafuni huishia ukingoni, hatua za Chemwor hazikumpeleka mbali kwa vile alitiwa nguvuni baada ya siku chache.

Sasa amezuiliwa katika korokoro ya kituo cha polisi cha Buruburu atakapotuliza visingino hadi siku 14 zikamilike.

Atashtakiwa kwa mauaji kisha azuiliwe aidha katika gereza kuu la Kamiti ama lile la Viwandani kusubiri uamuzi wa mwisho. Akipatikana na hatia huenda akafungwa jela maisha ama korti iamuru atiwe kitanzi kwa mujibu wa sheria.

Mshukiwa alisikika akighairi akisema “laiti ningelijua singekubali kutawaliwa na hisia za kimahaba na tamaa ambayo imeleta hasara kuu katika familia yetu.”

  • Tags

You can share this post!

Mkuu wa hospitali aamriwa amfikishe Sonko kortini

Wasichana mitaani waonywa dhidi ya ndoa za mapema