• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Wasichana mitaani waonywa dhidi ya ndoa za mapema

Wasichana mitaani waonywa dhidi ya ndoa za mapema

NA SAMMY KIMATU

MATHARE, NAIROBI

WASICHANA wameshauriwa kuzingatia umuhimu wa elimu badala ya kujiingiza katika ndoa za mapema na kubeba mimba za mapema.

Hayo yalinenwa mwishoni mwa wiki na mkurugenzi wa Wakfu wa Mathare, Bw Eric Omwanda Nehemiah. Alikuwa katika mkutano na vijana zaidi ya 1,000 katika mtaa wa mabanda wa Mathare.

Bw Eric aliongeza kwamba kabla ya kuelekea katika harakati za uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020 ni vyema kwa vijana kubadili kasumba ya kutumiwa vibaya na wanasiasa.

“Tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2022, msikubali kutumiwa na wanasiasa kuzua vurugu na ghasia kama tulivyoshuhudia miaka ya hapo awali. Badala yake, jiungeni na vikundi vinavyojihusisha na miradi ya maendeleo, ‘’ Bw Eric asema.

Katika kipindi cha mwaka mmoja tangu janga la Corona kuripotiwa nchini Kenya, wakfu wa Mathare ulisimama na vijana hao katika masuala ya kusaidia jamii katika mtaa huo.

Wakishirikiana na mashirika mbalimbali, vijana kutoka wakfu huo walishiriki zoezi la kupatiana barakoa, sabuni na vitakasa mikono kwa jamii ya Mathare na mitaa mingine katika kaunti ya Nairobi.

Vilevile, wakfu huo uliwanusuru wasichana watatu ambao walikuwa wameolewa wakiwa shuleni.

“Tuliwatembelea wasichana hao pamoja na maafisa wa utawala na maafisa wa kushughulikia masuala ya watoto na tukafanikiwa kuwarudisha shuleni wasichana watatu,’’ Bw Eric akaongeza.

Ili kuhakikisha vijana wanakuza talanta zao kando na masomo, wakfu huo una mradi wa talanta na michezo ikiwemo soka ya wasichana na ya wavulana.

Fauka ya hayo kuna pia usanii wa uimbaji pamoja na upigaji picha miongoni mwa vitengo vingine.

‘’Vijana wote hukutana kila jumapili kupiga msasa mambo kadhaa kwa minajili ya kusonga mbele na kusahau mambo ya mihadarati na usherati miongoni mwa watoto wetu,’’ Bw Eric akadokeza.

  • Tags

You can share this post!

Azuiliwa kwa kumuua nduguye wakipigania mwanamke

Madrid wapigwa breki na Sociedad