• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Seneti yapinga mbinu ya serikali kusaka mgao wa Sh370 bilioni kwa kaunti

Seneti yapinga mbinu ya serikali kusaka mgao wa Sh370 bilioni kwa kaunti

Na CHARLES WASONGA

HUENDA serikali ikalazimika kuwaongezea Wakenya mzigo wa ulipaji ushuru zaidi ili kuiwezesha kuzitengea serikali Sh370 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2021/2022.

Hii ni baada ya maseneta kukataa pendekezo la Waziri wa Fedha Ukur Yatani la kubadilisha Sh9.7 bilioni zitakazotengewa kaunti kama ruzuku ya kufadhili ukarabati wa barabara hadi kuwa fedha za kugawanywa baini ya kaunti zote 47. (equitable share).

“Tumepinga pendekezo hilo la Waziri wa Fedha kwa sababu hazina hiyo ya ukarabati wa barabara ilibuniwa kupitia sheria za bunge na kubadilishwa kwa pia kutahitajika kutekelezwa kupitia mageuzi ya sheria,” akasema Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Fedha Charles Kibiru.

Hazina hiyo ya kufadhili ukarabati wa barabara ilianzishwa katika mwaka wa kifedha wa 2014-2015 na pesa hizo zikatolewa kwa kaunti kama ruzuku mahsusi (conditional grants).

Ilibuniwa kupitia mabadiliko yaliyofanyiwa Sheria ya Bodi ya Barabara (KRB).

Pesa za hazina hiyo ni miongoni mwa ruzuku nne mahsusi ambazo serikali inalenga kubadilisha ili kuwa ili kupata fedha za mgao wa usawa wa Sh370 bilioni. Hatua hiyo itaiwezesha serikali kupata jumla ya Sh17.3 bilioni zaidi za kutoa kama mgao kwa kaunti ilivyopendekezwa kwenye Mswada wa Ugavi wa Mapato 2021 (DORA).

Pesa hizi pia zinajumuisha fedha ambazo serikali za kaunti hupokea kwa ajili ya kuimarisha vyuo vya mafunzo ya kiufundi mashinani.

Endapo Wizara ya Fedha itasalimu amri ya seneti basi italazimika kusaka pesa zaidi za mgao kwa kaunti kwa kuongeza viwango vya ushuru.

Kulingana na mswada wa ugavi wa mapato, serikali kuu inapendekeza kuwa mgao kwa kaunti uongezwe kutoka Sh316.5 bilioni za sasa hadi Sh370 bilioni katika mwaka ujao wa kifedha wa 2021/2022.

You can share this post!

‘Firirinda’ yapata umaarufu wa kipekee lakini...

Mswada kudhibiti mikopo ya kidijitali waandaliwa