• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
Kositany asema ataishtaki Jubilee kwa kumtimua

Kositany asema ataishtaki Jubilee kwa kumtimua

Na SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Soy Caleb Kositany amesema atachukulia hatua chama tawala cha Jubilee (JP) kwa kile anadai ni kumtimua kutoka wadhifa wake bila kufuata sheria.

Bw Kositany amesema hayo siku moja baada ya JP kumvua wadhifa wa naibu katibu mkuu wa chama.

Nafasi yake ilipokezwa mbunge wa Cherangany, Bw Joshua Kutuny.

Jubilee inasema ilichukua hatua hiyo inayotaja ni ya kinidhamu, kwa sababu ya Kositany kutoheshimu sheria na mikakati ya chama.

Kositany ni kati ya wabunge na wanasiasa ambao wameonekana kujiunga na chama cha UDA, kinachohusishwa na Naibu wa Rais Dkt William Ruto.

Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto amesema kufurushwa kwake kutakuwa funzo kwa timuatimua inayoshuhudiwa JP, anayotaja kuwa haramu.

“Lazima nichukue hatua ili wajue sheria zinapaswa kufuatwa,” Bw Kositany akasema.

Mwaka uliopita, 2020 JP iliwavua mamlaka viongozi kadha wa bunge la kitaifa na seneti wanaoegemea kundi la Tangatanga linalohusishwa na Naibu wa Rais Dkt Ruto.

Viongozi hao ni pamoja na mbunge wa Garissa Mjini Bw Aden Duale, ambaye alikuwa kiongozi wa wengi bunge la kitaifa, seneta wa Elgeyo Marakwet Bw Kipchumba Murkomen (kiongozi wa wengi seneti), seneta wa Nakuru Susan Kihika (kiranja wa wengi seneti), kati ya wengineo.

“Kutimuliwa kwangu ni njama ya kuendelea kutoa marafiki wa Naibu Rais. Waliofurushwa awali, sheria hazikufuatwa. Jubilee inaiga uongozi wa kimabavu wa chama cha ODM, ambapo wa kusema ni mtu mmoja,” Bw Kositany akadai.

Huku mbunge huyo akishikilia kwamba ataendelea kukosoa Rais Uhuru Kenyatta anapokosa, uhusiano wa kiongozi wa nchi na naibu wake unazidi kudorora.

Dkt Ruto amekuwa akidai tangu Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga wazike tofauti zao za kisiasa Machi 2018 kupitia salamu za maridhiano maarufu kama Handisheki, anatengwa katika serikali.

Naibu mwenyekiti wa Jubilee, Bw David Murathe alionya Jumanne kwamba chama hicho kitaendelea kuadhibu viongozi wanaokiuka sheria za chama.

You can share this post!

Msanii ‘Lonely Man’ awaumbua mabinti wapenda...

Hatuogopi mswada wa kumtimua Ruto serikalini – Kositany