• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Man U watamaushwa na sare ya Palace

Man U watamaushwa na sare ya Palace

Na MASHIRIKA

MATUMAINI finyu ya Manchester United kushinda ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu yalididimizwa hata zaidi mnamo Machi 3, 2021 baada ya kulazimishiwa sare tasa na Crystal Palace uwanjani Selhurst Park.

Licha ya kuchezea ugenini, Man-United walimiliki asilimia kubwa ya mpira ila wakashindwa kutumia vyema nafasi nyingi za wazi walizozipata kupitia kwa Nemanja Matic na Bruno Fernandes waliomweka kipa Vicente Guaita katika ulazima wa kufanya kazi ya ziada.

Palace hawakuweza kuelekeza kombora lolote langoni mwa wageni wao hadi mwanzoni mwa kipindi cha pili wakati ambapo fowadi Jordan Ayew aliposhirikiana vilivyo na mshambuliaji Christian Benteke na kumtia kipa Dean Henderson kwenye shughuli.

Nusura Palace wafungiwe bao la dakika za mwisho kupitia kwa Patrick van Aanholt japo akashindwa kujaza mpira kimiani licha ya kusalia peke yake na kipa Henderson.

Sare hiyo inaamanisha kwamba Man-United kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 51 huku pengo la pointi 14 likitamalaki kati yao na viongozi Manchester City watakaowaalika ugani Etihad mnamo Machi 8, 2021.

Kwa upande wao, alama moja iliyovunwa na Palace katika mechi hiyo iliwasaza katika nafasi ya 13 kwa alama 34 sawa na Wolves. Ni pengo la pointi 11 sasa ndilo linawatenganisha na Fulham ambao kwa pamoja na West Bromwich Albion na Sheffield United, wako katika mduara wa vikosi vilivyoko katika hatari ya kuteremshwa ngazi mwishoni mwa kampeni za msimu huu.

Baada ya kuchuana na Man-City, ratiba ngumu ya Man-United itaendelea dhidi ya AC Milan ya Italia kwenye hatua ya 16-bora ya Europa League kabla ya kushuka dimbani kupepetana na Leicester City kwenye robo-fainali za Kombe la FA.

Japo Man-United wamepoteza mechi moja pekee ligini tangu Novemba 1, 2020, masogora hao wa kocha Ole Gunnar Solskjaer wameshuhudia michuano yao mingi ya hivi ikikamilika kwa sare.

Palace watakuwa wageni wa Tottenham Hotspur katika mchuano wao ujao wa EPL mnamo Machi 8, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Sheffield yapiga Aston Villa katika EPL licha ya kusalia na...

Udinese wadidimiza matumaini ya AC Milan kutwaa taji la...