• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 12:15 PM
Malala alia kuna wizi wa kura Matungu

Malala alia kuna wizi wa kura Matungu

Na SAMMY WAWERU

SENETA wa Kakamega Cleophas Malala amesema chama cha ANC hakitakubali matokeo ya kura ya eneobunge la Matungu, Kaunti ya Kakamega, kufuatia uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika Alhamisi.

Bw Malala amedai vituo 20 vimeshuhudia udanganyifu mkubwa wa kura. Seneta huyo amesema ODM imesakata njama ya kuchakachua kura, kuhakikisha mgombea wa chama hicho, Bw Paul Were ametwaa kiti cha ubunge.

Chama cha ANC na kinachoongozwa na Bw Musalia Mudavadi, kimeshiriki zoezi hilo la kidemokrasia, Bw Oscar Nabulindo akipeperusha bendera.

UDA, chama kinachohusishwa na Naibu wa Rais, Dkt William Ruto kimewakilishwa na Bw Alex Lanya.

Huku shughuli za upigaji kura Matungu zikiendelea, seneta Malala ameibua tetesi kwamba chama cha ODM kimewahonga wapigakura kwa pesa.

Vilevile, Malala amelalamikia hatua ya wafuasi wa ODM kuruhusiwa kuingia vituoni wakiwa wamevalia kofia zenye nembo ya chama, akidai wengine hawana vitambulisho, na kwamba ni njama (kuvalia kofia ya chama) iliyopangwa ili washiriki kuchagua Bw Were.

Aidha, ameendelea kueleza kuwa baadhi ya vituo vya kupigia kura vilifungwa mapema hata kabla wakati wa kukunja jamvi zoezi hilo haujatimia.

“Nimetazama stakabadhi za vituo hivyo vinaonyesha mgombea wa ODM anaongoza ilhali upigaji kura unaendelea. Isitoshe, maafisa wa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) wameandika uchaguzi ulikamilika saa nane na dakika arubaini na moja, mchana,” Dkt Malala akaambia wanahabari, akionyesha stakabadhi za vituo ambavyo hakuvitaja, upigaji kura umekamilika na kura kuhesabiwa.

“Maafisa wa polisi tayari wamekamata baadhi ya wahusika waliokuwa wakihonga wapiga kura…Tunataka zoezi hili lisitishwe mara moja. Hatutakubali matokeo,” akawaka seneta huyo.

Hali tete ilishuhudiwa Matungu, kufuatia madai hayo ya udanganyifu, Bw Malala akiambia wanahabari kwamba aliporwa kima cha Sh2 milioni mbili alizosema zilikuwa kwenye gari lake.

Wakati huohuo, aliyekuwa Waziri wa Michezo, Bw Rashid Echesa amejipata pabaya baada ya kumzaba kofi afisa mmoja wa IEBC.

Kiti cha ubunge Matungu kilisalia wazi baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge, Bw Justus Murunga (ANC) kuaga dunia Novemba 2020.

You can share this post!

Echesa akamatwe mara moja – Chebukati

Sonko anaugua maradhi ya ubongo na moyo, hawezi kuendelea...