• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 10:21 AM
‘Tuliangusha BBI kuadhibu gavana’

‘Tuliangusha BBI kuadhibu gavana’

EVANS KIPKURA na BARNABAS BII

MADIWANI wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet walikataa kuidhinisha mswada wa kubadilisha katiba wa Mpango wa Maridhiano (BBI) ili kumhujumu Gavana Alex Tolgos kwa kutomuunga Naibu Rais William Ruto.

Gavana huyo na seneta wa Kaunti hiyo Kipchumba Murkomen wanashindana kudhibiti siasa za kaunti hiyo kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Madiwani hao walisema kwamba kuteuliwa kwa Bw Tolgos na Rais Uhuru Kenyatta kuongoza kampeni za BBI hakukufurahisha viongozi wengi wa eneo hilo na wakazi.

“Tulipokea simu kutoka kwa watu wengi wakituambia tuunge mswada huo. Walitutusi lakini tulishikilia msimamo wetu,” alisema diwani wa wadi ya Kapyego Musa Limo.

Mwenzake wa wadi ya Soi North, Bw Zack Magut alisema kwamba bunge la Kaunti lilisikiliza wakazi kabla ya kukataa kupitisha mswada huo. Inasemekana kuwa Murkomen aliwashawishi madiwani 17 waliopiga kura kukataa mswada huo mnamo Jumanne. Ni madiwani 15 waliopiga kura kuunga mswada huo.

Bw Tolgos alimtaka Naibu Rais William Ruto na washirika wake “kukoma kuwapotosha wakazi wa Rift Valley kwamba BBI inalenga kumzuia kuingia ikulu.”

“Ni muhimu kwa watu wetu kuelewa kwamba kuchanganya siasa za urithi za 2022 na BBI hakutatupeleka mahali, ni sharti tueleze watu wetu kwamba kubadilisha katiba au BBI ni tofauti na urithi wa Rais Kenyatta, hapo ndipo tunapotea kama eneo,” Bw Tolgos alisema.

“Tumejihusisha na siasa nyingi eneo hili. Tukizungumzia BBI, sio ya kugawana nyadhifa, tunapoambia watu wetu kwamba tunapeleka asilimia 35 ya mapato kwa serikali za kaunti, kitakachofuata baada ya hilo hakina maana,” aliongeza.

“Seneta wa eneo hili anafahamu vyema kwamba kaunti inapokea pesa chache sana kutoka kwa serikali ya kitaifa lakini amekuwa akipiga kelele Nairobi akipinga mswada ambao utaletea kaunti pesa zaidi, huu ni ubinafsi,” Bw Tolgos alisema majuzi.

Mwaka jana, Gavana Tolgos alimlaumu seneta Murkomen kwa kuwatumia madiwani kumtisha baada ya madiwani kupinga pendekezo la kupunguza bajeti ya bunge la Kaunti ya ShSh566 milioni ili kujaza pengo la Sh200 milioni katika bajeti ya serikali ya kaunti.

Bw Tolgos alihama kambi ya Dkt Ruto mnano Mei mwaka jana akilaumu washirika wa naibu rais akiwemo Murkomen, wabunge Caleb Kositany (Soy), Oscar Sudi (Kapseret) na msaidizi wake Farouk Kibet kwa dharau na kutotambua wadhifa anaoshikilia katika Kaunti.

Bw Murkomen amemlaumu Gavana Tolgos kwa kutomuunga Dkt Ruto katika azima yake ya kisiasa.

Anasema kwamba Bw Tolgos amekuwa akihujumu viongozi wanaomuunga Dkt Ruto.

You can share this post!

Wazee Kisumu wataka serikali iwarejeshee joka lao la Omieri

Mwandishi wa NMG, Pauline Ongaji atuzwa