• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Wakenya washangaa mbona Uhuru, Ruto na Raila hawajapokea chanjo ya corona

Wakenya washangaa mbona Uhuru, Ruto na Raila hawajapokea chanjo ya corona

Na MARY WANGARI

SERIKALI mnamo Ijumaa, Machi 5, 2021, ilizindua rasmi kampeni ya kusambaza chanjo ya Covid-19 kote nchini huku hisia mbalimbali zikiibuka miongoni mwa Wakenya.

Wakenya walijitosa katika mtandao ya kijamii wa Twitter huku wakiashiria hisia mseto kuhusu chanjo hiyo aina ya AstraZeneca, iliyowasili nchini mnamo Jumanne usiku.

Hatua ya Dkt Patrick Amoth kupokea chanjo hiyo kama Mkenya wa kwanza na mhudumu wa afya wa kwanza hasa ilibwaga zani na kuzidisha shaka miongoni mwa wanamitandao.

Wengi walishangaa ni kwa nini Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto , kiongozi wa ODM Raila Odinga au hata Waziri wa Afya Mutahi Kagwe hawakuongoza kupokea chanjo hiyo kama kielelezo bora kwa raia.

Walitilia shaka ufaafu na usalama wa dozi hizo zaidi ya milioni moja za AstraZeneca, wakisisitiza kuwa ni sharti viongozi wakuu nchini wawe mstari wa kwanza kuipokea jinsi inavyotendeka katika mataifa mengine.

“Ili kuchochea imani kuhusu ufaafu na usalama wa chanjo hiyo, tunapaswa kuanza na viongozi wakuu jinsi tulivyoshuhudia katika mataifa mengine,”

“Ni muhimu sana! La sivyo huenda wamepokea chanjo yenye ubora wa hali ya juu, hii ni Kenya,” alihoji Kyalo Musembi.

“Fedha za Covid-19 zilipoingia viongozi wakuu serikalini walikuwa wa kwanza kunufaika, natarajia kwamba watakuwa wa kwanza kunufaika kutokanana chanjo,” alisisitiza Bicholus Yong.

“Nilitarajia Uhuru, baraza lake na wabunge kuwa wa kwanza kupokea chanjo,” alishangaa Jason Mutua.

Wengine waliashiria kukosa imani na serikali kuhusiana na usalama na ufaafu wa chanjo hiyo.

“Sina imani kabisa na serikali. Nijikute,” alisema Muchina “Siipendi. Inakaa kuwa na nia fiche,” Boaz Omari alisema.

“Tusubiri tuone kitakachomtendekea kwanza kabla ya kwendea yetu mwaka ujao,” Alley

Kunao waliokaribisha uzinduzi huo wa chanjo wakiutaja kama mwanzo wa mwisho wa kuzingatia masharti ya Wizara ya Afya kuhusu kujikinga na virusi vya corona.

“Curfew itolewe Sasa tupige sherehe,” alisema Marvin Baha. “Hebu kidogo. Baada ya chanjo bado tunahitaji kujitenga kijamii na stori za kuvalia barakoa?” alishangaa Martha Mwarama.

Uzinduzi wa chanjo hiyo aina ya AstraZeneca katika Hospitali Kuu ya Kenyatta, ulijiri karibu mwaka mmoja tangu kisa cha kwanza cha Covid-19 kiliporipotiwa nchini Kenya mnamo Machi 13, mwaka uliopita.

Akizungumza baada ya kupokea chanjo hiyo, Dkt Amoth aliwahakikishia Wakenya kuwa chanjo hiyo ni salama na kuwahimiza kujiandaa kuipokea.

You can share this post!

Dkt Patrick Amoth Mkenya wa kwanza kupata chanjo ya corona

Hatimaye Echesa atiwa nguvuni