ODM: Raila anachezwa

Na VICTOR RABALLA

WAANDANI wa kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, wamedai kuwa wapo watu wenye ushawishi serikalini wanaopanga kuteua mtu atakayeongoza taifa hili, ambaye si waziri huyo mkuu wa zamani, baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuhitimisha hatamu yake.

Wakiongozwa na Seneta James Orengo (Siaya), washirika hao ambao pia walisema kuna kundi linalopanga kuuteka mchakato wa kurekebisha katiba kupitia mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI), walidai njama hizo zinaendeshwa na watu wa karibu wanaomzunguka Rais Uhuru.

Bw Orengo alidai watu hao tayari wameamua taratibu zitakazotumiwa katika kuendesha mchakato huo na uchaguzi mkuu wa 2022.

“Wameteka hata utaratibu mzima wa BBI ili wauendeshe kutoka afisi za serikali,” akasema.

Seneta huyo akidai kuwa watu hao washaamua ni nani atakayeongoza nchi baada ya Rais Uhuru kung’atuka uongozini mwaka ujao, alisema, “Kama ilivyofanyika wakati Rais Mstaafu Mwai Kibaki alipokuwa akihudumu muhula wake wa pili mnamo 2013, baadhi ya watu serikalini wanajaribu kubuni mkakati wa kumrithi Rais Kenyatta,” akasema.

Wandani wa Bw Odinga walitishia kuwataja watu hao, akisema wanaongozwa na ubinafsi katika kujaribu kubuni njia ambapo taifa hili litatawaliwa.

Bw Orengo, ambaye pia ndiye Kiongozi wa Wachache kwenye Seneti, alionya kuhusu athari za njama hizo, akisema hilo ni sawa na kuingilia uhuru wa Wakenya kufanya maamuzi yao kwa njia huru.

“Tunawarai wafanyakazi hao na polisi kujiepusha na njama hizo na badala yake kuzingatia taasisi za kikatiba,” akasema kiongozi huyo, aliyekuwa akihutubu katika eneo la Asembo, Kaunti ya Siaya.

Bw Orengo alidai kuwa kwa miezi mitatu hadi minne iliyopita, maafisa hao wamekuwa wakijaribu kuingilia utekelezaji wa miradi muhimu kwa kuingiza siasa.

“Wakati wafanyakazi wa serikali wanajaribu kuingilia mwelekeo wa nchi kwa maslahi yao ya kibinafsi, nchi haiwezi kuwa na amani. Wanavuna pale ambapo hawakupanda. Bila handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga ambayo imeleta amani, hawangekuwa wakipanga njama hizo,” akasema.

Mbunge wa Rarieda, Otiende Amollo, aliwaomba wafuasi wa Bw Odinga kumuunga mkono kwenye azma yake ya kuwania urais 2022, akieleza imani kwamba ataibuka mshindi.

“Wakati huu, tuna mbinu ambayo wamekuwa wakiitumia. Tunayajua yote, hivyo msiwe na wasiwasi kuhusu njama za baadhi ya watu,” akasema.

Kauli sawa na hiyo ilitolewa mnamo Ijumaa kwenye runinga moja na kakake Bw Odinga, Dkt Oburu Oginga, aliyedokeza kuwa huenda Bw Raila akaamua kushirikiana na Naibu Rais William Ruto hapo 2022 iwapo atatemwa na Rais Uhuru.

“Uvumi huo nimeusikia lakini nado sijauthibitisha wala hakuna mipango kama hiyo kwa sasa. Lakini katika siasa lolote lawezekana,” akasema kaka huyo mkubwa wa Bw Raila.

Bw Otiende Amollo alisema ana imani Bw Odinga ‘hatanyang’anywa’ ushindi wake kama ilivyofanyika kwenye chaguzi za 2007, 2013 na 2017.

Mwakilishi wa Kike wa Siaya, Dkt Christine Ombaka pia aliisifia ripoti ya BBI, akisema itawainua wanawake kwa kuwapa nyadhifa nyingi za kisiasa.

“Wanawake wanapaswa kuwania nafasi mbalimbali wala hawapaswi kungoja kupewa nyadhifa hizo hivyo tu,” akasema.

Rais Kenyatta na Bw Odinga walianza mchakato wa BBI mnamo 2018 kama njia ya “kurejesha uthabiti wa kisiasa nchini”.

Wakenya wanatarajiwa kushiriki kwenye kura ya maamuzi baadaye mwaka huu, baada ya zaidi ya mabunge 40 ya kaunti kuipitisha ripoti hiyo.

Tayari, mswada kuhusu ripoti ya BBI ushawasilishwa kwenye Seneti na Bunge la Kitaifa ili kujadiliwa.

Kulingana na utaratibu uliowekwa, maamuzi ya mabunge hayo hayatakuwa na athari zozote kwa mswada huo, hilo likimaanisha ni wazi kura hiyo itaandaliwa.

Habari zinazohusiana na hii

Vigogo wapimana akili

UHURU AMTULIZA RAILA

Wababaisha ‘Baba’