• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
Uhuru aamuru ardhi ya KDF irejeshewe jamii ya Samburu

Uhuru aamuru ardhi ya KDF irejeshewe jamii ya Samburu

Na GEOFFREY ONDIEKI

RAIS Uhuru Kenyatta ameamuru kuhamishwa kwa kituo cha mafunzo ya Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kutoka maeneo ya Lkuroto na Lpartuk katika eneo la Samburu ya Kati hadi Baragoi, Samburu Kaskazini.

Kiongozi wa taifa mnamo Ijumaa alitoa hatimiliki za ardhi ambazo zamani zilitumika katika maeneo ya mafunzo kwa wanajeshi wa KDF.

“Tunaendelea na mpango wetu wa kutoa hatimiliki na umiliki wa maeneo ya Lpartuk na Lkuroto utarejeshewa wenyeji mara moja. Kuanzia sasa wanajeshi watahamia eneo la Baragoi,” Rais alisema.

KDF na Serikali ya Kaunti ya Samburu zimeachilia ardhi za KDF Lkuroto na Lpartuk ili kukomesha mzozo wa miongo kadhaa baina yake na wakazi wa maeneo hayo.

Ardhi hiyo yenye ukubwa wa ekari 3,000 iliyoko viungani mwa mji wa Maralal ilitengewa KDF katika eneo la kuendeshea mafunzo ya kijeshi katika miaka ya 1970. Hata hivyo, wakazi waliivamia na kujenga makazi.

Vipande hivyo vya ardhi (Lkuroto na Lpartuk) vilitengewa KDF kupitia notisi katika Gazeti rasmi la serikali nambari 3,210 toleo la Novemba 11, 1977.

Kama hatua ya kusitisha mzozo kati ya wakazi na serikali kuhusu ardhi hizo, Rais Kenyatta alisema eneo la Lpartuk litarejeshwa kwa jamii na eneo la Lkuroto litageuzwa kuwa sehemu ya mji wa Maralal.

Serikali ya Kaunti ya Samburu imetoa ekari 1,000 katika eneo la Baragoi itakayotumika kama eneo la mafunzo ya kijeshi.

Rais Kenyatta alisema kuhamishwa kwa ardhi ya jeshi kutawezesha upanuzi wa mji wa Maralal ambao unakuwa kwa haraka kutokana na ujenzi wa barabara ya lami kutoka Rumuruti hadi Maralal.

You can share this post!

Mitihani ya kitaifa ya Gredi 4 yaanza Jumatatu

Kaunti yaanza kuwalipa fidia wakazi wa Buxton