• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
DINI: Tuwe kama bundi; tuutumie usiku ‘kuona’ yale ambayo wengi hawaoni

DINI: Tuwe kama bundi; tuutumie usiku ‘kuona’ yale ambayo wengi hawaoni

NA PADRE FAUSTIN KAMUGISHA 

Mimi ni bundi wa usiku, alisema Barak Obama, rais wa 44 wa Marekani. Kwa maneno hayo tunaalikwa kutumia vizuri usiku kama bundi.

Bw Barak Obama kadiri ya mahojiano na mwandishi wa habari mwaka 2009 alibainisha kuwa analala saa 6.30 usiku. Saa za usiku hujishughulisha na kuandika na kusoma. Oprah Winfrey huenda kitandani saa nne usiku na kuamka saa kumi na mbili asubuhi.

Akihojiwa na mwandishi wa habari mwaka 2017 alisema, “Kwa kawaida naenda kitandani nikiwa na shajara kubwa za shukrani karibu nami kitandani. Jambo la mwisho ambalo nafanya kabla ya kulala naandika mambo matano ambayo yamenipa raha kubwa au ambayo ninashukuru.”

Kabla ya kulala hesabu baraka na kumshukuru Mungu. Tuige mazuri ya bundi. Katika tamaduni nyingi za Kiafrika bundi ni mtabiri misiba, majanga na vifo. Lakini bundi ana mazuri yake.

“Bundi ni ndege mwenye busara sana kati ya ndege wote kwa sababu anaona mengi zaidi na kusema machache” (Methali ya Kiafrika).

Kwa mtazamo chanya tuseme na mtunga Zaburi, “Nimekuwa kama ndege wa jangwani, na kufanana na bundi katika mahame” (Zaburi 102:6).

Ingawa bundi katika mahame ana shida lakini katika giza nene unaweza kuona nyota vizuri. “Watu wanasema gizani ndipo siri nyingi zimejificha. Muda wa usiku unaleta uwazi na umakini kwa bundi,” alisema Kimberly Morgan.

Hapa tunasisitiza matendo mema yakufanyika usiku. Kwa mtazamo chanya bundi ni ishara ya machale yaani kuchezwa machale, ishara ya uwezo wa kuona lile ambalo wengine hawaoni, subira, hekima na busara. Bundi ni ishara ya kuona nyuma ya pazia ya vinyago ambavyo baadhi ya watu huvaa.

“Kimapokeo bundi ni ishara ya hekima, hivyo sisi si njiwa bali ni bundi, na tunakesha wakati wengine wamelala,” alisema Urjit Patel.

Usiku unaweza kufanya mambo mengi mazuri. Unaweza kutafakari juu ya Mungu usiku.

Mtunga Zaburu anatushauri, “Ninapokukumbuka kitandani mwangu na kutafakari wewe makesha yote ya usiku” (Zaburi 63:6). Ukiwa kitandani tafakari neema na baraka za Mwenyezi Mungu.

Elon Reeve Musk Mkurugenzi wa kampuni iitwayo Space X hugusa mto wa kulalia saa saba usiku. Huamka saa moja asubuhi.

Anatumia kipindi cha usiku kutafakari na kufanya kazi. Alizaliwa tarehe 28 Juni, 1971 huko Pretoria, Afrika ya Kusini. Kwa sasa ana uraia wa Marekani. Utajiri wake ni dola za Kimarekani bilioni 190. Anajulikana kwa kuanzisha makampuni mawili: Tesla Motors na Space X. Akiwa na umri wa miaka 24 alianzisha kampuni iitwayo Zip2 Corporation.

Bill Gates mwanzilishi wa kampuni ya Microsoft anasisitiza kulala muda walau masaa 7 kwa siku.

Alisema, “Najisikia vizuri siku nzima nikiwa usiku nimelala masaa 7.” Bill Gates kabla ya kulala anatumiaa moja kusoma vitabu. Kwa ufupi watu waliofanikiwa wanalala masaa 6-7 usiku lakini wanautumia muda vizuri kabla ya kulala. Kuna hadithi juu ya nyota ya asubuhi na nyota ya jioni.

Nyota ya asubuhi ilitamba kuwa ina umuhimu mkubwa. Inawaangazia wachapakazi asubuhi kuchapakazi. Nyota ya jioni nayo ilijigamba kuwa inawaangazia wachapakazi jioni kufanya kazi yao wakfurahia mwanga. Jua lilijitokeza na kusema,

“Nyote mnafanya kitu kile kile:kuwaangazia wachapakazi kwa vipindi tofauti.” Kwa ufupi wachapakazi wanaamka mapema. Wachapakazi wanautumia vizuri muda wa usiku.

Muda wa usiku ni wakati mzuri wa kutafakari, kuandika, kupanga ya kesho, kuwa na maono, kuota ndoto za maendeleo.

You can share this post!

Kaunti yaanza kuwalipa fidia wakazi wa Buxton

DOUGLAS MUTUA: Uchina isipime corona kwa njia ya...