Chanjo ya corona isiwe cheti kuamsha ufuska

NA BENSON MATHEKA 

Kupatikana kwa chanjo ya corona kumechangamsha watu ambao wamekuwa wakisusia ufuska wakihofia huenda wakaambukizwa virusi hivyo.

Kote ulimwenguni, watu waliopata chanjo hiyo, wamekuwa wakitupia picha zao wakichanjwa kwenye mitandao ya kijamii na kuandika jumbe za mapenzi.

Wataalamu wa masuala ya kijamii na mapenzi wanasema kwamba lengo lao ni kutangaza kuwa wamepata kinga ili kurudia maisha yao ya kawaida ikiwemo ya ufuska.

“Watu walijikausha kwa kuhofia kuwa wangeambukizwa virusi. Baada ya chanjo kupatikana sasa wanataka kuonyesha kuwa wamepata kinga ya kufufua maisha yao ya ufuska,” asema Devon Greyson, mwanasaikolojia na mtafiti wa masuala ya jamii.

Anasema kwamba watu wanafaa kufahamu kuwa kupata chanjo hakumaanishi kwamba maisha yanarejea kama kawaida mara moja.

“Chanjo ya corona sio cheti cha kurudia vituko vya ufuska. Hapana, ni mwanzo tu wa safari ndefu ya kukabiliana na janga ambalo lilibadilisha maisha ya mapenzi ya watu wengi kote ulimwenguni,” asema Devon.

Wataalamu wanasema kwamba wanaoweka picha zao kwenye mitandao ya kijamii wakichanjwa zikiambatana na ujumbe wa mapenzi wanalenga kualika watu kwa ufuska.

“Habari kuhusu chanjo na tendo la ndoa bado hazijabainishwa. Corona husambazwa kupitia mfumo wa kupumua na hii inafanya tendo la ndoa shughuli hatari sana. Inafaa kubainika kuwa hakuna chanjo inayotoa kinga ya asilimia moja na utafiti wa awali unaonyesha kuwa watu wanaopata chanjo pia wanaweza kuambukiza wengine ambao hawajaipata,” asema Devon.

Hata hivyo, wataalamu wanasema kwamba inaweza kuwa salama kwa watu wawili waliopata chanjo kurambishana asali kuliko aliyepata chanjo kuburudishana na ambaye hajapata.

“Inaweza kuwa salama kwa watu wawili waliochanjwa kurambishana asali wakitumia mbinu salama kwa sababu bado kuna hatari ya kuambukizwa maradhi mengine,” asema.

Wanasaikojia wanasema kwamba wengi walisitisha ufuska huku wataalamu wa afya wakiendelea kusisitiza umuhimu wa kudumisha umbali na kuvalia barakoa kama njia ya kuzuia kuambukizwa na kusambaza virusi vya corona.

Ushauri wa wataalamu wa afya umefanya wengi kukaukiwa na uroda hadi chanjo ilipopatikana wakaichangamkia.

“Haiwezekani kwa mtu asiye na mchumba wa kumpunguza joto kuishi kama mtawa. Hii ndiyo sababu kupatikana kwa chanjo kumechangamkiwa na wengi na hata kutangaza mitandaoni wakiipata huku wakiambatisha picha na jumbe za mapenzi,” asema Debra Murithi wa shirika la Maisha Mema jijini Nairobi.

Chanjo dhidi ya virusi hivyo ilianza kutolewa nchini wiki hii na wengi wanasema itawasaidia kurudia maisha yao ya ufuska.

“Ukweli ni kwamba nimekuwa na hofu ya kushiriki ufuska lakini sasa, chanjo hii itaniondolea hofu baada ya kuvumilia kwa miezi saba,” asema David Bosire, 30, mkazi wa Nairobi ambaye bado kapera.

Bosire ambaye hana mpenzi anakiri kwamba alikuwa akila ufuska na vidosho tofauti kabla ya janga la corona kuripotiwa nchini yapata mwaka mmoja uliopita.

“Nilikuwa nimekawia kuoa lakini sasa nitajipanga. Kama ningekuwa na mke singekaukiwa hivi,” asema na kuongeza kuwa yuko tayari kugharimika kupata chanjo hiyo.

Kulingana na Beta Aloo, mkazi wa mtaa wa South C, Nairobi, chanjo itamfanya arudie maisha yake ya mapenzi.

“Nilisitisha starehe zangu na burudani kwa sababu ya hofu ya kuambukizwa corona. Nitapata chanjo na kurudia maisha niliyokuwa nikifurahia kabla ya Machi 13 mwaka jana,” aeleza mwanadada huyu.

Anasema kwamba hatakubali kushiriki ufuska na mwanamume ambaye hatakuwa amechanjwa.

“Nimeumia kwa mwaka mmoja ambao nimekuwa nikivumilia kwa hofu ya kuambukizwa corona. Sitakubali kuhusiana na mwanamume ambaye hatachanjwa,” aeleza.

Aloo anasema japo amekuwa akienda kazini, amekuwa akiepuka vitendo vya ufuska na uroda.

Hata hivyo watalaamu wanaonya watu kuwa waangalifu hata baada ya kupata chanjo wakisema ni mapema kusherehekea.

Habari zinazohusiana na hii