• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
JAMVI: Ruto, Raila wanavyojinadi kutumia miradi ya wandani

JAMVI: Ruto, Raila wanavyojinadi kutumia miradi ya wandani

Na LEONARD ONYANGO

NAIBU Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga sasa wanatumia mbinu mpya kujipendekeza kwa wapigakura huku kampeni za kinyang’anyiro cha urais 2022 zikishika kasi.

Viongozi hawa wawili wamekuwa wakikimbilia kuzindua miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na wandani wao katika maeneo mbalimbali nchini ili kujipigia debe.

Baada ya kutengwa na kuzuiliwa kukagua miradi ya serikali, Dkt Ruto ambaye leo anamalizia ziara yake ya siku tatu katika Kaunti ya Meru, amekimbilia kukagua na kuzindua miradi inayotekelezwa na wabunge na magavana wanaoegemea mrengo wake, makanisa na kutoa mabasi kwa shule na makundi ya vijana.

Katika muda wa siku 30 zilizopita, Naibu wa Rais amekagua na kuzindua zaidi ya miradi kumi katika maeneo ya Magharibi, Bonde la Ufa na Mlima Kenya.

Wiki iliyopita, Dkt Ruto alizindua miradi mbalimbali katika kaunti ya Narok, ikiwemo ufunguzi wa kiwanda cha maziwa cha Oseketeti Le Kule kilichoko katika eneo la Naikarra. Mradi huo ulijengwa kupitia ufadhili wa fedha zilizotengewa Wawakilishi wa Wanawake (NGAAF).

Mwakilishi wa wanawake wa Narok Soipan Tuya ni miongoni mwa wandani wa Ruto.

Akiwa katika Kaunti ya Narok, Dkt Ruto alitoa basi kwa Shule ya Sekondari ya Ilmotiook iliyoko katika eneobunge la Narok Magharibi.

Naibu wa Rais aliekea Narok siku chache baada ya kuzuru eneobunge la Gatanga, Kaunti ya Murang’a ambapo aliongoza mikutano ya kuchangisha fedha kwa ajili makundi 30 ya wahudumu wa bodaboda katika miji ya Kihumbuini na Kirwara.

Februari 26, alikuwa katika eneobunge la Endebess , Kaunti ya Trans Nzoia, ambapo alizindua jumba la maakuli la Shule ya Sekondari ya Kitum.

Mbunge wa Endebess Robert Pukose ni miongoni mwa wabunge ambao wamekuwa wakipigania kuhakikisha kuwa Dkt Ruto anaingia Ikulu baada ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Mwezi uliopita, Naibu wa Rais pia alizindua miradi mbalimbali katika eneo la Bonde la Ufa ambalo ni ngome yake ya kisiasa. Miongoni mwa miradi aliyozindua katika eneo hilo ni kituo cha afya cha Kobujoi kilichoko mjini Kapsabet, Kaunti ya Nandi.

Dkt Ruto alizuru Kaunti ya Nandi baada ya kutoka Kaunti ya Baringo ambapo alizindua vibanda katika soko la Kabarnet.

Alipozuru katika eneo la Pwani, mnamo Januari, mwaka huu, Dkt Ruto alizindua miradi mbalimbali iliyotekelezwa na wandani wake, ikiwemo Shule ya Msingi ya Kwa Bullo na Shule ya Sekondari ya Kwa Bullo katika eneobunge la Nyali linaloongozwa na Mohamed Ali.

Katika Kaunti ya Kwale, Dkt Ruto alizindua Kituo cha Polisi cha Mwangulu kilichojengwa na Fedha za Hazina ya Ustawishaji Maeneobunge (NG-CDF) ya Lunga Lunga linaloongozwa na Khatib Mwashetani.

Kwa upande wa Bw Odinga, amekuwa pia akizindua miradi iliyotekelezwa na wandani wake akijiandaa kwa ajili ya kinyang’anyiro cha urais.

Jumatano, Bw Odinga alizindua Shule ya Msingi ya Tsangalaweni, Kaunti ya Kilifi. Ujenzi wa shule hiyo ulifadhiliwa na fedha za NG-CDF zinazosamimiwa na mbunge wa Ganze Teddy Mwambire ambaye ni mwandani wake.

Jumanne, alizindua jengo la darasa katika Shule ya Msingi ya Mwakinyungu katika eneobunge la Mwatate lake Andrew Mwadime.

Bw Odinga pia alizindua ujenzi wa soko la kisasa la Mwatate.

Kiongozi wa ODM pia amekuwa akizindua miradi mbalimbali katika maeneo ya Nyanza ambayo ni ngome yake ya kisiasa. Mradi wa hivi karibuni ni ufunguzi wa Chuo cha Mafunzo ya Utabibu (KMTC) cha Ugunja, Kaunti ya Siaya.

Aidha, Bw Odinga amekuwa akiahidi baadhi ya maeneo kuwa atapeleka malalamishi yao kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa mbinu hizo zinasaidia viongozi hao kuonekana wachapakazi.

“Wabunge au magavana wanaalika vinara wao kuzindua miradi yao ili waonekane kwamba wamefanya kazi. Vilevile, wanatoa fursa kwa vinara wao kujionyesha kwamba ni wachapakazi,” asema Bw Mark Bichachi aliye mdadisi wa masuala ya kisiasa.

You can share this post!

Chanjo ya corona isiwe cheti kuamsha ufuska

MAUYA OMAUYA: Serikali idhibiti wanabodaboda, vinginevyo...