• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 10:55 AM
MAUYA OMAUYA: Serikali idhibiti wanabodaboda, vinginevyo tutajuta

MAUYA OMAUYA: Serikali idhibiti wanabodaboda, vinginevyo tutajuta

Na MAUYA OMAUYA

Siku moja taifa hili litagutuka na kupata miji na vijiji vimetekwa na magenge yanayojulikana wazi lakini serikali itakuwa imepoteza uwezo wa kuyang’oa au kuyadhibiti kikamilifu.

Haya ni magenge ya vijana wa bodaboda wanaozidi kupenyeza mizizi yao katika barabara na mitaa kote nchini. Sekta hii kwa sasa inachipukia popote bila maelekezo ya kitaaluma au mwongozo wa sheria unaolainisha biashara na utendakazi wao.

Ramli za wachanganuzi zinaonyesha kwamba tunakoelekea, sekta hii itageuka kuwa jinamizi la usalama na kuleta majuto kwa jamii. Jukumu kuu la serikali yoyote duniani ni kuhakikisha kwamba maisha katika mipaka yake yanaendeshwa kulingana na taratibu za kisheria na maelekezo yanayokubalika kwenye jamii husika.

Ilivyo nchini Kenya kwa sasa, serikali imeshindwa au imejitia hamnazo katika juhudi za kulainisha uwepo wa bodaboda barabarani. Kila siku mpya sekta hii inakua kwa haraka na licha ya kuwa kitega uchumi kwa wahusika, sekta hii pia imechochea maovu na kuleta madhara yanayoatua nyoyo za wengi.

Zaidi ya Wakenya milioni 14 hutumia mbinu hii ya usafiri kila siku.

Kuna yapata bodaboda nusu milioni za kibiashara kwenye barabara zetu na pato la kila siku kwa wahusika ni takriban Sh450 milioni.

Katika nchi ambako uchechefu wa hela na uhaba wa ajira ni janga, inaeleweka kwa urahisi kwa nini biashara hii imewavutia maelfu ya vijana.

Hata hivyo sekta hii sasa inaelekea kuwa chimbuko la maovu iwapo serikali haitatia guu chini, kuilainisha na kuiweka ndani ya mabano ya sheria.

Mwanzo ni ukiukaji wa taratibu za usalama barabarani, jambo ambalo limesababisha vifo vingi ambavyo vingeepukika.

Kufikia sasa ajali za bodaboda huua idadi kubwa ya watu barabarani kushinda magari, jambo ambalo halingedhaniwa miaka michache iliyopita.

Ukitembelea hospitali nyingi nchini utapata wodi iliyotengewa majeruhi wa ajali za bodaboda. Hali yao ni ya kuhuzunisha sana.

Taswira ya misongamano ya bodaboda katikati mwa miji na barabarani inachukiza mno na inachangia mazingira duni na hali mbovu ya hewa.

Wanaotembea kwa miguu na waendeshaji magari hukumbana na madhila ya bodaboda hawa ambao wamenyakua kila nafasi barabarani. Wepesi wa kupenya na kuhepa huwapa fursa ya kuvunja sheria za barabarani bila kujali matokeo.

Majuma mawili yaliyopita walichukua sheria mikononi mwao na kuteketeza gari la naibu gavana wa Kisii, Joash Maangi baada ya kuhusika kwenye ajali eneo la Narok. Kufikia sasa wahusika hawajashtakiwa. Mijini na vijijini, pikipiki hizi zimegeuzwa vyombo vya kutekeleza uhalifu na kisha kutoweka kwa haraka.

Kufikia sasa hakuna mfumo mwafaka wa serikali kuhakikisha kwamba kila mwanabodaboda amesajiliwa rasmi, ana ujuzi, stakabadhi zifaazo na kituo rasmi cha kutekeleza biashara na vifaa vyote vinavohitajika.

Ukosefu wa udhibiti umeruhusu magugu kuota katika shamba hili. Umefungua lango kwa wahalifu kujificha humo na baadhi ya polisi kusherehekea rushwa inayozidisha uozo na maangamizi kwenye jamii.

Vijana wengi wanaoacha masomo wameambulia kwenye sekta hii kwa sababu ya urahisi wa kuingia na ukosefu wa taratibu rasmi.

Hata ushuru wanaotakiwa kulipa unayeyuka tu kwa sababu ya kuzembea kwa serikali.

Imebainika pia vijana husika wanatumiwa visivyo katika ulanguzi wa mihadarati, wahamiaji haramu, usafirishaji wa magaidi na kutekeleza mikwaruzano ya kisiasa na wanasiasa.

Ukuaji wa makundi haramu kama Mungiki au ghasia za bodaboda barabarani unawezekana tu kufuatia ulegevu wa serikali iliyopuuza majukumu yake.

Sekta ya bodaboda imesambaa kote nchini kama moto nyikani. Ukosefu wa udhibiti na mwongozo thabiti wa sheria umefanya bodaboda kugeuka jinamizi kila ujao.

Tusipoziba ufa, tutajenga ukuta halafu!

[email protected]

You can share this post!

JAMVI: Ruto, Raila wanavyojinadi kutumia miradi ya wandani

BENSON MATHEKA: Wagombeaji wa kiume wazuiwe kuwadhalilisha...