• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 2:10 PM
CHARLES WASONGA: Wakuzaji kahawa wapate hamasisho kuhusu kanuni mpya

CHARLES WASONGA: Wakuzaji kahawa wapate hamasisho kuhusu kanuni mpya

Na CHARLES WASONGA

KUTUPILIWA mbali kwa kesi iliyopinga utekelezaji wa mageuzi mapya katika sekta ya kahawa ni hatua ya kuchangamkiwa, sababu inatoa nafasi kwa mazungumzo kuhusu njia bora za kufufua sekta hiyo.

Baadhi ya wanachama wa mashirika ya kahawa walipinga kanuni hizo mpya, zinazofahamika kama Crops (Coffee) General Regulations 2019, kwa sababu mbalimbali.

Kanuni hizo zilichapishwa na serikali mnamo 2019. Wanachama hao, ambao ni wakulima wa kahawa, haswa walipinga sehemu ambazo, kwa mfano, zinapendekeza pesa za mauzo ya kahawa kuwekwa katika akaunti za mashirika husika kabla ya wao wakulima kusambaziwa.

Pia walidai kanuni hizo “zinakiuka Katiba”. Lakini wiki jana Jaji wa Mahakama Kuu Weldon Korir alitupilia mbali malalamishi ya wanachama hao ambao wengi wanatoka eneo la Kati.

Kufuatia uamuzi huo wa mahakama, serikali na wadau wengine katika sekta sasa wamepata fursa ya kushirikiana pamoja katika juhudi za kufufua sekta ya kahawa ambayo imedorora.

Itakumbukwa kwamba katika miaka ya 1980s sekta ya kahawa ilikuwa imenawiri, kiasi kwamba wakulima nchini wangezalisha karibu tani 130,000 kila mwaka.

Kiwango hicho cha uzalishaji sasa kimeshuka hadi tani 40,000 kwa mwaka kutokana na changamoto mbalimbali.

Hizi ni kama vile usimamizi mbaya wa vyama vya ushirika vya wakulima, utendakazi na usimamizi duni wa viwanda vya kahawa, wizi wa kahawa na kudorora kwa bei katika masoko ya humu nchini na kimataifa.

Takwimu kutoka Wizara ya Kilimo zinaonyesha kuwa wakulima wadogo ndio wameathirika zaidi.

Baadhi wamelazimika kung’oa mikahawa yao na kuwekeza katika ukuzaji wa mimea mingine, kama vile mboga na matunda ambayo yanawapa pato nzuri.

Waziri wa Kilimo Peter Munya sasa aweke mikakati itakayohakikisha kuwa wakulimu wamepewa hamasisho la kina kuhusu kanuni hizo mpya, ambazo zinalenga kuwakinga wakuzaji kahawa dhidi ya ulaghai wa madalali na wafanyabiashara wengine matapeli.

Hii ni kwa sababu baadhi ya wakulima wamekiri kutofahamu kwa kina manufaa ya kanuni hizo kwao, ilhali ndio wadau wakuu katika sekta ya kahawa.

Wizara inaweza kuendesha ufahamu huo kupitia vyama vya ushirika vya kahawa nchini.

Vile vile, maafisa wa vyama wanapaswa kuwafundisha wakulima jinsi ya kukopa Sh3 bilioni za Hazina ya Mkopo kwa Wakulima wa Kahawa, iliyotolewa na serikali kuwapiga jeki wakuzaji zao hilo.

Imebainika kuwa baadhi ya wakulima hawafahamu jinsi ya kuwasilisha maombi ya kupokea fedha hizo za mkopo, ambao hutozwa riba ya chini.

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Raia wasipotoshwe na siasa za...

FAUSTINE NGILA: Tujizoeshe maisha ya dijitali