• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:55 PM
Bandari iko tayari kulima Nzoia Sugar

Bandari iko tayari kulima Nzoia Sugar

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

KOCHA wa Bandari FC, Andre Cassa Mbungo amesema kuwa watakuwa wakitumia mbinu mbalimbali kulingana na timu watakayokuwa wakikutana nayo huku akieleza matumaini ya timu yake kupata ushindi itakapocheza na Nzoia Sugar kwenye mechi ya Ligi Kuu ya FKF hivi leo uwanjani Mbaraki Sports Club.

Mbungo anasema wanasoka wake wako imara na wako tayari kuhakikisha wamepata ushindi kuzidisha matumaini yao ya kupanda ngazi hadi kufikia kilele cha ligi hiyo. “Tunakutana na Nzoia tukiwa wakati tunafanya uzuri na tunataka tuendelee kupata ushindi na kuongeza matumaini ya kuwa kileleni mwa ligi,” akasema.

Nahodha wa timu hiyo, Bernard Odhiambo alisema yeye na wenzake wako tayari na wana hamu ya wakati ufike kwa pambano lao la nyumbani litakalofanyika hivi leo na Nzoia Sugar hapo uwanja wa Mbaraki Sports Club.

“Sisi wachezaji tuko imara na tuna hamu ya kutaka kushinda mchezo wetu na Nzoia. Tunaamini kwa mafunzo ya wakufunzi wetu, tutafanikiwa na tuna tamaa ya kuondoka uwanjani tukiwa washindi,” akasema Odhiambo.

Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa Bandari FC, Twahir Muhiddin amesema ana imani kubwa ya timu yake hiyo kufanya vizuri kwenye ligi kuu ya mashindano mengine kwa sababu wachezaji ni wasikilifu na wenye kucheza kwa ari ya kuipatia timu yao ushindi.

Akiongea wakati wa kutangazwa rasmi kwa naibu kocha mpya wa timu hiyo Anthony Kimani hapo Mbaraki Sports Club juzi Alhamisi, Muhiddin alisema anavutia mno na jinsi wachezaji walivyokuwa na umoja miongoni mwao na kushirikiana na maofisa wao wa benchi la ufundi.

“Navutiwa mno na umoja walionao wachezaji wetu na nia ya kuipenda timu yao na hayo mawili ni viungo muhimu vinavyoweza kuisaidia timu yetu kufika mbali na kufanikiwa kwa malengo yake yakiwemo ya kubeba kombe la ligi kuu,” akasema Muhiddin.

Naye mkufunzi wa magolikipa Wilson Obungu amesema amefurahikiwa kufanya kazi na makocha waliobobea na wenye uzoezi ambao utaisaidia Bandari kuendeleza ubabe wake katika ligi ya msimu huu.

Anasema wana nia kubwa na malengo ya kuifanya Bandari iendelee kuwa mojawapo ya klabu zenye uwezo mkubwa wa kushinda mashindano ya hapa nchini na kupata tikiti ya kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa.

You can share this post!

Kiungo Matt Ritchie aomba msamaha kwa kumchemkia kocha wake...

Nabulindo aahidi kuunganisha wakazi wa Matungu