• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
Nzoia, Bandari Zagawana Pointi Kwenye Mechi ya Ligi Kuu

Nzoia, Bandari Zagawana Pointi Kwenye Mechi ya Ligi Kuu

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

TIMU ya Nzoia Sugar FC jana iliondoka na alama moja ya Ligi Kuu ya Betway (BPL) baada ya kuilazimisha Bandari FC kutoka sare ya kufungana bao 1-1 kwenye mechi kali iliyochezwa uwanja wa Mbaraki Sports Club mjini Mombasa Jumamosi Machi 6, 2021.

Nzoia ilianza mchezo huo kwa kasi na kulivamia lango la wenyeji lakini ilibidi wasubiri hadi dakika ya 20 ndipo ilipopata bao la kuongoza lilofungwa kwa njia ya penalti na Gabriel Wandera baada ya mchezaji mwenzake Felician Okanda kufanyiwa faulo mbaya na kipa Justin Ndakumana.

Mbali na penalti hiyo Nzoia ilinufaika na uamuzi wa refarii Wilson Otieno alipompa kadi nyekundu beki wa Bandari, Brian Otieno kunako dakika ya majeruhi ya kipindi cha kwanza.

Ilikuwa kwenye kipindi cha pili ndipo Bandari iliingia ikiwa imeazimia kusawazisha bao hilo na kufunga mengine lakini ukuta wa Nzoia ukilindwa vyema na Gabriel Wanders.

Ian Karani wa Nzoia alipewa kadi nyekundu kunako dakika ya 54 baada ya kumfanyia faulo mbaya Abdalla Hassan. Bandari iliweza kusawazisha bao hilo kwenye dakika ya 70 wakati Amani Atariza alipotuma krosi iliyomkuta William Wadri aliyetuma kombora hadi wavuni.

Kocha wa Bandari FC, Andre Cassa Mbungo alisema vijana wake walifanya makosa katika kipindi cha kwanza yaliyosababisha kufungwa bao katika kipindi cha kwanza lakini alipofanya mabadiliko, walicheza vizuri kipindi cha pili bna kuweza kusawazisha.

“Kiuhakika wachezaji wangu walizubaa katika kipindi cha kwanza na ndipo waliwapa fursa wapinzani wetu kujipatia bao lao, lakini mabadiliko ya kipindi cha pili yalichangamsha na kuweza kupata bao la kusawazisha,” akasema Mbungo.

Naye kocha wa Nzoia ambaye aliwahi kuwa naibu kocha wa Bandari, Ibrahim Shikanda aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza soka la hali ya juu na kuondoka na alama moja ilikuwa ni mafanikio.

“Wanasoka wangu ambao walipata ushindi dhidi ya Gor na kutoka sare na Bandari, wamefanya kazi kubwa na tuna uhakika tutakapokutana na Ulinzi Stars nyumbani kwetu, tuna tamaa ya kubeba pointi zote tatu,” akatamba Shikanda.

Aliyekuwa mchezaji aliyetemwa na Bandari, Moses Mwale aliweza kucheza vizuri na kuwazuia washambuliaji wa timu yake hiyo ya zamani. “Ninashukuru kurudi Mombasa na kufanikiwa kucheza vizuri dhidi ya timu yangu ya zamani na kuisaidia timu yangu mpya kuondoka na pointi moja,” akasema Mwale.

You can share this post!

Mwatate yajiandaa kuonyesha ubabe wake Kisumu Jumatatu

Wabunge 10 waitwa na NCIC kuhusu fujo