• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Dkt Immanuel Gitamo: Mwanajeshi kutoka Kitale anayepiga jeki juhudi za SpaceX ya Elon Musk, Amerika

Dkt Immanuel Gitamo: Mwanajeshi kutoka Kitale anayepiga jeki juhudi za SpaceX ya Elon Musk, Amerika

CHRIS WAMALWA Na SAMMY WAWERU

TANGU hadithi ya ufanisi wa Dkt Emmanuel Gitamo ifichuke kupitia Jarida la The US Army mwezi uliopita, Februari 2021, Wakenya wanaoishi Marekani wameeleza kuridhishwa kwao na jinsi mwanajeshi wa Amerika na ambaye ni raia wa Kenya, ameweza kukwea katika kikosi cha kijeshi chenye umaarufu na ushawishi mkuu ulimwenguni, chini ya muda mfupi.

Kwa wengi, ni fanaka kutoka kiwango cha chini, ufukara hadi kuwa mkwasi, hadithi inayoshiria na kueleza bayana dhana “Marekani chochote kinawezekana”.

Wanaamini Dkt Gitamo amefanikisha ndoto zake katika nchi yenye ushawishi mkuu duniani, ndiyo Amerika.

Kinachostaajabisha wengi, mbali na kuwa mwanajeshi wa kwanza wa rangi nyeusi (asili ya Kiafrika) katika kikosi cha Jeshi la Marekani aliyefuzu kwa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Masuala ya Unajimu (Astrophysics – Mafundisho yasiyo ya Kisayansi kuhusu uhusiano kati ya nyota na maisha hapa duniani), Dkt Gitamo ni kiungo muhimu kufanikisha mradi wa Falcon 9 ulioanzishwa na SpaceX, roketi zinazoweza kutumika tena.

“Kazi yangu ilikuwa kuhakikisha vigezo vyote vinaafikiwa,” Dkt Gitamo akasema kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali.

Hilo linaenda sambamba na kuingiana na nyanja yake, Unajimu.

Kulingana na Dkt Mukurima Muriuki, mtafiti Mkenya jimbo la California, ambaye pia alipata fursa ya kumhoji afisa huyo wa kijeshi Amerika, asilimia 1.2 ya raia wa Marekani wana Shahada ya Uzamivu, kiwango cha elimu kinachokadiriwa kuwa na chini ya asilimia 2 ya wasomi kote duniani.

“Kwa mujibu wa takwimu hizo, ni maajabu Mkenya kuwa kwenye asilimia mbili ya wasomi wenye Shahada ya Uzamivu ulimwenguni, ikizingatiwa kuwa wazazi wake hawakuwa na uwezo kifedha. Wasingeweza kukimu karo ya shule bora Nairobi.

“Hakufuzu masomo ya shule ya upili pekee, ila amepata Shahada za Digrii, Uzamili na Uzamivu kutoka Taasisi ya Teknolojia ya California (CIT) na pia kujiunga na Kikosi cha Jeshi la Marekani,” Muriuki akaelezea kwenye chapisho lake la majuzi katika jarida la kila wiki la African Warrior Magazine, (AW Magazine).

Wasomaji wengi walichangia maoni na kusema ufanisi wa Dkt Gitamo unatokana na bidii alizotia na pia bahati.

Ni habari njema za Mkenya huyo, ambazo zimekuwa zikisambaa mitandaoni baada ya kuchapishwa na Jarida la US Army.

Dkt Gitamo, binafsi anaamini safari yake ya ufanisi maishani ni miujuza.

Alisema shabaha kueleza hadithi ya ufanisi wake kwa ulimwengu, ililenga kuwapa motisha vijana Wakenya na Afrika kwa jumla, wanaoishi Amerika kwamba pia wao wanaweza kufanikiwa.

“Ninatilia mkazo kauli ya dadangu staa Lupita Nyong’o, Marekani ni rahisi kufanikisha ndoto zako. Ni nchi yenye nafasi za mafanikio kila mahali. Unachohitaji ni kuangaza na kupepesa macho yako mbali, na kukumbatia fursa zilizopo. Ni muhimu vijana tunaoishi humo tujue ufanisi Marekani unatokana na kujiunga na shule na kusoma kwa bidii,” Dkt Gitamo akahimiza.

Akiwashauri vijana, afisa huyo msomi anawataka kufahamu kinaga ubaga haijalishi msingi au hali ya familia waliyozaliwa ama kutoka.

Kilele, ni muhimu kukumbatia neema anazokupa Mungu na nafasi za ufanisi anazokujaalia.

Anasema, kupitia imani ya maombi na bidii, yeyote yule anaweza kuafikia matarajio na ndoto zake maishani.

Kufikia sasa, DKT Gitamo, ndiye mwanajeshi wa kipekee katika kikosi cha US Army kufuzu na kuwa na Shahada ya Uzamivu katika Masuala ya Unajimu.

Dkt Immanuel Gitamo, ambaye ni opareta wa kikosi cha kijeshi cha wana anga, akiwa na mamlaka ya Brigedia wa daraja la 2, Divisheni ya Pili ya Kikosi cha Pamoja cha Lewis-McChord, jijini Washington, alizaliwa na kulelewa eneo la Kitale, Kaunti ya Trans Nzioa.

Kwenye mahojiano, Dkt Gitamo alichelea kufukua safari ya maisha yake utotoni, kwa kile alihoji “ni ya kuhuzunisha na kusikitisha kuyakumbuka”.

‘Wazazi’ waliomlea, hata hivyo hawakuridhia yaliyofukuliwa na Jarida la US Army.

Alifichua kwamba mahojiano na jarida hilo, yalieleza bayana magumu na mazito aliyopitia nchini Kenya kabla ya kuhamia Marekani.

“Wazazi walionizaa walinitupa pamoja na kaka yangu tukiwa wadogo kiumri, hivyo basi siwajui,” Dkt Gitamo alidokeza. Pamoja na ndugu yake, walilelewa kama mayatima eneo la Kitale.

“Tulipatikana tumeachwa kandokando mwa barabara na wazazi waliotuzaa,” akaelezea, akiongeza kwamba hajui babake wala mamake mzazi.

Dkt Immanuel Gitamo (kushoto), mwanajeshi Mkenya anayefanya kazi katika kampuni ya utafiti wa sayari SpaceX, Amerika. Picha/ Chris Wamalwa |

Walichukuliwa na wanandoa waliowakumbatia na kuwalea. Kulingana na simulizi ya Dkt Gitamo, maisha hata hivyo hayakuwa rahisi, kwani wazazi hao waling’ang’ana kuwapa lishe na pia kuwasomesha, kwa sababu hawakuwa na uwezo vile kifedha.

Aliambia Jarida la US Army, alivalia viatu kwa mara ya kwanza alipofikisha umri wa miaka 14. Walimu katika shule aliyosomea, walielewa hali yake, hivyo basi walimruhusu kusoma bila kulipa karo.

Dkt Gitamo anataja ukarimu huo kama ni miujiza, na ndio maana aliamua kujitolea kufanyia shule hiyo kazi bila malipo.

“Kufanikisha chochote kile maishani, niligundua ni muhimu kuwa na imani ya Mungu na pia kutia bidii. Nilikuwa nikisoma hata baada ya kila mtu kulala usiku, na ninakiri nimeafikia yale ambayo wengi wamekuwa wakitamani,” akasema.

Kuhamia Amerika na kufuzu kwa Shahada mbalimbali

Baada ya kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE, mwaka wa 2006, alipata kibali kuhamia Amerika (Green card), ambapo aliendeleza hamu ya kukata kiu chake cha masomo.

Alifuzu kwa Shahada ya Digrii, Masuala ya Uhandisi wa Sayansi ya Anga na Shahada ya Uzamili, Masuala ya Uhandisi wa Sayansi ya Fizikia ya Nyuklia kutoka Taasisi ya Teknolojia ya California (CIT), taasisi ambayo ni miongoni mwa vyuo vitano bora duniani.

Kulingana na Dkt Mukurima Muriuki, mtafiti Mkenya jimbo la California, CIT husajili chini ya asilimia 2 pekee ya wanaoomba nafasi.

Dkt Gitamo anatafsiri Sayansi ya anga kama kuwa na nidhamu mara mbili za uhandisi.

Ya kwanza ni uhandisi wa anga, unaozingatia ndege zilizoko angani. Pili, ni uhandisi wa anga unaozingatia chochote kilichoko nje ya Sayari ya Dunia.

Hivyo basi, Shahada yake ya Digrii inaangazia utafiti, ubunifu, Sayansi na teknolojia inayoshughulikia utengenezaji wa ndege na kuzifanyia majaribio.

“Hivyo ndivyo nilijipata kuorodheshwa katika mradi wa Spacex Falcon 9, ambao umezinduliwa mara 107. Umefanikisha roketi kutua mara 67 na kupaa mara 50. Aidha, 2027 SpaceX ni mpango tunaoendelea kushughulikia na unaotarajiwa kuenda Sayari ya Mirihi (ya nne katika mfumo wa Jua, na jirani ya Dunia),” akafafanua.

Ni kupitia mradi huo, Dkt Gitamo alipata fursa ya kipekee kukutana na Mhandisi tajika aliyetamani kutangamana naye na ambaye ana asili ya Kiafrika, Elon Musk.

Bw Musk ni mwasisi wa mradi wa SpaceX na pia kampuni ya Paypal, inayowezesha wateja kufanya malipo kupitia Intaneti.

Akitumia mfano wa tajiriba ya Mhandisi huyo, Dkt Gitamo anasema vijana wa Kafrika wanapaswa kujua malengo makuu maishani yanajiri kupitia bidii na maono.

“Kwa sasa ninakuza vijana wenye uraia wa Kenya eneo la Seattle (Washington, Amerika) ambao wanajiandaa kuchagua taaluma watakazosomea. Tayari, nimeona wameanza kufa moyo kwa sababu hawajui kozi bora kuchagua. Ni muhimu tuwaongoze na kuwapa ushauri nasaha,” akaelezea Afisa huyo.

Alifichua kwamba, nchini Kenya amejituma kutoa msaada kwa shule na makanisa.

Vilevile, Dkt Gitamo anafadhili masomo ya wanafunzi kadha, akidokeza kuwa hivi karibuni atazindua mpango wa kusaidia jamii, kama njia mojawapo kuridhia baraka za Mwenyezi Mungu.

Safari ya milima na mabonde

Licha ya ufanisi aliopata, anasema haijakuwa safari ya mteremko.

Kila hatua, nilituma barua za maombi na kutia bidii. Kufuzu kwa Shahada ya Uzamivu haijakuwa rahisi. Inahitaji nidhamu na ustahimilivu wa hali ya juu. Baada ya sala, Mungu alinifungulia milango ya heri na fanaka, ndiye mimi huyu sasa nina Shahada ya Uzamivu katika Masuala ya Unajimu (Astrophysics),” akasema.

Dkt Gitamo anaweza kusimulia siku nzima kuhusu Unajimu. Anasema ni kitengo cha Sayansi ya anga, inayotumia sheria za Fizikia na Kemia kueleza kuzaliwa, maisha na ‘kufariki’ kwa nyota, Sayari, Galaksi, nebula, kati ya vifaa vinginevyo ulimwenguni.

“Kama Wanajimu, hutaka sana kuelewa kuhusu ulimwengu. Mapenzi ya anga ndiyo yalinishikiza kusomea kozi nilizokumbatia,” akasema.

Anasema alichagua kujiunga na kikosi cha Kijeshi cha Amerika ili apate ufadhili wa masomo kuafikia ndoto zake maishani na mahitaji mengineyo.

Alifuzu kwa Shahada ya Uzamivu katika Masuala ya Unajimu mwaka wa 2019, na anafichua kwamba kwa sasa anasomea Shahada ya Uzamivu katika Masuala ya Fizikia ya Atomiki.

Huku akisalia na miezi michache kuondoka katika kikosi US Army, anasema analenga kuchambua zaidi kozi ya masuala ya anga, “kwa kuwa asilimia kubwa ya kila tunachofanya inahusishwa na anga”.

Mapenzi yake katika anga ni bayana kutokana na tafiti alizofanya na anazoendelea kufanya, utunzi na michango anayotoa katika nyanja hiyo.

Kama Wakenya wengi wenye malengo, Dkt Gitamo ana maono makuu na ambaye bidii naye ni kama chanda na pete, ili kuyaafikia.

Anaamini bidii huondoa kudura, na zaidi ya yote kumhusisha Maulana katika kila jambo na hatua, kwa njia ya maombi.

Kufikia hii leo, ameafikia ndoto zake. Wengine watasema nyota alizolenga amezifikia, na bila shaka amezikumbatia.

You can share this post!

Duka la Nakumatt linavyohudumia wateja kisiri Nairobi

Mbappe abeba PSG hadi ndani ya 16-bora French Cup