• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
TAHARIRI: Serikali isubire ripoti kuhusu AstraZeneca

TAHARIRI: Serikali isubire ripoti kuhusu AstraZeneca

KITENGO CHA UHARIRI

CHANJO ya Corona ilipozinduliwa rasmi wiki jana, kuna Wakenya walioelezea wasiwasi wao kuhusu chanjo hiyo aina ya AstraZeneca, ambayo iliwasili nchini mnamo Jumanne usiku.

Baadhi walishangaa ni kwa nini Kaimu Mkurugenzi wa Wizara ya Afya, Dkt Patrick Amoth ndiye aliyekuwa wa kwanza kupokea chanjo hiyo badala ya Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto au hata Waziri wa Afya Mutahi Kagwe waliostahili kuongoza kama kielelezo bora.

Wapo waliotilia shaka ubora na usalama wa dozi hizo zaidi ya milioni moja za chanjo hiyo, wakisisitiza kuwa ni sharti viongozi wakuu nchini wawe mstari wa kwanza kuipokea jinsi inavyotendeka katika mataifa mengine.

Wakenya hao pengine hawakuwa na nia yoyote mbaya dhidi ya viongozi wao, bali walitarajia wapewe maelezo zaidi kuhusu usalama wa kutumia chanjo hiyo.

Na siku moja baada ya shauku zao, wagonjwa wawili walifariki dunia nchini Korea Kusini baada ya kudungwa chanjo hiyo. Mkurugenzi wa Shirika la Kudhibiti Maradhi Korea Kusini, Jeong Eun-kyeong alisema nchi yake inachunguza iwapo kuna uhusiano wowote kati ya chanjo hiyo na vifo vya raia wake wawili.

Na jana, serikali ya Austria ilisimamisha utumizi wa chanjo hiyo baada ya kifo cha mwanamke wa miaka 49 na kuugua ghafla kwa mtu mwengine wa miaka 35.

Gazeti la Niederoesterreichische Nachrichten liliripoti kuwa wanawake wote wawili (aliyekufa na aliyeugua baada ya kudungwa chanjo hiyo) walikuwa wauguzi katika kliniki eneo la Zwettl.

Inawezekana kuna sababu tofauti za watu hao kufariki au kuugua na huenda watakaodungwa hapa Kenya wasiwe na dalili kama hizo. Chanjo ya AstraZeneca imewasili kwenye kaunti mbalimbali na wahudumu wa afya pamoja na wadau wengine watadungwa leo Jumatatu.

Dkt Amoth aliwahakikishia wananchi kwamba chanjo hiyo ni salama na akawahimiza wajiandae kuipokea. Lakini matukio ya nchini Korea Kusini na Austria hayafai kupuuzwa.

Serikali yapaswa kusubiri ripoti ya uchunguzi wa visa hivyo viwili kwanza kuhusu chanjo hiyo, kabla ya kuendelea nayo kwa raia wake. Iwapo itakuwa salama kwa wanadamu, basi hakutakuwa na wasiwasi wowote kwa wananchi kuitumia.

Tumeisubiri chanjo kwa karibu mwaka mmoja tangu kisa cha kwanza kitangazwe nchini. Kusubiri kwa siku chache zaidi hakutakuwa na madhara yoyote.

You can share this post!

Usalama: Masomo yatatizika Baringo

Manchester United wapiga Manchester City breki kali ligini