Ajuta kupeleka kesi kwa wakwe

Na JOHN MUSYOKI

KITENGELA, Kajiado

HATUA ya kalameni wa hapa ya kumshtaki mkewe kwa wazazi wake iliambulia patupu alipoangushiwa kichapo kikali na wakwe zake kwa kumdhalilisha binti yao.

Inasemekana jamaa alimrudisha mkewe kwa wazazi wake na kudai alikuwa msumbufu kupindukia.

Siku ya kioja, wakwe wakimwalika jamaa kwenye kikao cha faragha ambapo polo alieleza kwamba demu hakuwa mke aliyetarajia wala kumfaa maishani.

“Sina furaha na ninasikitika sana kwa kuoa binti yenu. Tulipofanya harusi alibadilika ghafla. Nikimwambia kitu haambiliki. Haniheshimu kwa lolote. Mimi nimechoka kabisa. Sitakubali kukaliwa chapati na binti yenu kutaka kuwa kichwa katika boma yangu. Utundu huu wake ameutoa wapi? Nimechoka kuishi maisha ya presha,” jamaa alilalamika.

Inasemekana mzee alichemka na kumzima polo.

“Unaongea kwa ukali hapa kama nani? Hujui ni mimi mwenye boma na huyu ni msichana wangu. Kama umechoka na binti yetu wacha kumharibia jina. Binti yetu sio mtundu kwa sababu tulimlea kwa misingi ya kikristo. Kuna wanaume wanaommezea mate kama wewe umemchoka,” mzee wa boma alimwambia polo.

Polo alichemka zaidi na kuanza kumsuta mkewe mbele ya wazazi wake.

“Hautatoboa hata ukiolewa na mwanaume mwingine. Hakuna mwanaume atakayekuvumilia ukiwa na utundu huo wako wa kishetani. Wewe ni mtu bure kabisa,” jamaa alipayuka.

Inasemekana kabla ya jamaa kuendelea kumsimanga demu, wakwe walikerwa na maneno yake na kumtwanga bila huruma.

“Sitakubali uendelee kumtusi binti yangu mbele ya watu. Nitakuharibu hiyo sura yako,” mzee aliwaka huku akimtandika polo kwa bakora.

Jamaa alipozidiwa na maarifa alitoka shoti na kutorokea usalama wake.