Kocha Steven Gerrard aongoza Rangers kutwaa taji la Ligi Kuu ya Scotland kwa mara ya kwanza baada ya miaka 10

Na MASHIRIKA

RANGERS walitwaa ufalme wa Ligi Kuu ya Scotland mnamo Jumapili kwa mara ya kwanza baada ya kipindi cha miaka 10 baada ya waliokuwa mabingwa watetezi Celtic kuambulia sare tasa dhidi ya Dundee United.

Chini ya kocha Steven Gerrard ambaye ni kiungo na nahodha wa zamani wa Liverpool, Rangers walipepeta St Mirren 3-0 mnamo Jumamosi na sasa wanajivunia pengo la alama 20 kileleni zikisalia mechi sita pekee kwa kampeni za muhula huu kutamatika rasmi.

Taji la Ligi Kuu ya Scotland ni la kwanza kwa Gerrard kunyanyua tangu ajitose katika ulingo wa ukufunzi na kupokezwa mikoba ya Rangers ugani Ibrox miaka mitatu iliyopita. Ufanisi wa Rangers muhula huu unakomesha ukiritimba wa Celtic ambao wametawala soka ya Scotland kwa mfululizo wa miaka 10 iliyopita.

Isitoshe, ni mara ya kwanza kwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Scotland kupatikana mapema zaidi katika msimu zikisalia mechi sita zaidi kabla ya kampeni za muhula kutamatika rasmi.

Rangers wametwaa taji la Ligi Kuu ya Scotland wakijivunia rekodi ya kutoshindwa na wamepoteza alama nane pekee kufikia sasa. Ushindi dhidi ya St Mirren mnamo Jumamosi ya Machi 6, 2021 ulikuwa wao wa 28 kutokana na mechi 32 zilizopita.

Kikosi hicho kilicho na makao makuu mjini Glasgow kimefunga jumla ya mabao 77 na kimefungwa mabao tisa, mawili kati ya hayo yakiwa katika uwanja wao wa nyumbani wa Ibrox.

Rangers walikuwa wakikokota nanga mkiani mwa jedwali la Ligi Kuu ya Scotland mnamo 2012 baada ya hazina yao ya fedha kukauka. Ilikuwa hadi mwaka wa 2016 waliporejea kwenye kampeni za kuwania taji la Ligi Kuu.

Mechi ya kwanza itakayosakatwa na Rangers wakiwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Scotland ni Debi ya Old Firm itakayowakutanisha na Celtic ugenini, uwanjani Celtic Park, mnamo Machi 21, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO