Wanasiasa waanza kushtakiwa kwa vurugu chaguzini

Na WAANDISHI WETU

SENETA wa Kakamega Cleophas Malala na Mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro waliachiliwa Jumatatu kwa dhamana baada ya kujiwalisha kwa polisi kuhusiana na fujo zilizotokea katika chaguzi ndogo zilizofanyika wiki jana.

Naye Waziri wa zamani wa michezo Rashid Echesa aliendelea kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Gigiri hadi leo ambapo Mahakama ya Kiambu itatoa uamuzi ikiwa ataachiliwa kwa dhamana au la.

Bw Echesa alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Mahakama hiyo Bi Patricia Gichohi ambapo alishtakiwa kwa kudhulumu afisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) mnamo Machi 4, katika eneobunge la Matungu, Kakamega wakati wa uchaguzi wa marudio wa ubunge. Alikamatwa Ijumaa wiki jana baada ya kujiwasilisha kwa maafisa wa polisi mjini Mumias.

Akiongea baada ya kuachiliwa huru Jumatatu, Seneta Malala alisema aliitwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Kakamega kuhusu ghasia zilizokumba uchaguzi mdogo wa Matungu.

“Nilikuwa ajenti mkuu wa ANC katika uchaguzi huo na nimeelezea yote niliyofahamu kuhusu fujo.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Kakamega Hassan Barua alisema Bw Malala aliachiliwa huru kwa dhamana ya pesa taslim na akaamriwa kufika kortini kesho, Jumatano.

Naye Osoro, alikana mashtaka ya uharibifu wa mali siku ya uchaguzi mdogo wa Wadi ya Kiamokama, kaunti ya Kisii alipofikishwa mbele Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Kisii Nathan Shihundu

Uchaguzi huo uliofanyika Alhamisi wiki jana, ulikumbwa na ghasia ambapo walinzi wa mbunge huyo walikabiliana na kundi la vijana ambao ni wakosoaji wa Bw Osoro.

Kwenye mvutano huo, gari dogo la vijana hao lilibingiria na kuharibika walipokuwa wakitoroka, huku waliokuwemo wakijeruhiwa.

Kutokana na kisa hicho, polisi walianza kumsaka Bw Osoro. Lakini Jumatatu asubuhi alijiwasilisha mwenyewe kwa maafisa wa DCI, mjini Kisii.

Bw Osoro aliandamana na mawakili wake; mbunge wa Kandara Alice Wahome, Mbunge Mwakilishi wa Uasin Gishu Bi Gladys Boss miongoni mwa wengine. Wabunge hao ni wanachama wa vuguvugu la Tangatanga linaloongozwa na Naibu Rais William Ruto

Alikana madai ya madai ya kuchochea ghasia na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 au Sh 50,000 pesa taslimu. Kesi itatajwa Machi 22, 2021.

Mnamo Ijumaa wiki jana wabunge wanne wandani wa Dkt Ruto walishtakiwa katika mahakama ya Bungoma kwa tuhuma za kuzua ghasia wakati wa uchaguzi katika eneobunge la Kabuchai, kaunti ya Bungoma.

Hii ni baada ya wanasiasa hao; Didmus Barasa (Kimilili), Wilson Kogo (Chesumei), Nelson Koech (Belgut) na Seneta wa Nandi Samson Cherargei kukamatwa kwa madai kuwa magari yao yalibeba silaha, dalili kuwa walikuwa wakipanga kuzua fujo.

Wanasiasa hao ni miongoni mwa wale ambao walifika eneobunge hilo kuhudumu kama maajenti wa mgombeaji wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Evans Kakai.

Walikana makosa hayo na kuachiliwa huru kwa dhamani ya Sh50,000 pesa taslim na mdhamini ya Sh100,000. Kesi yao itasikizwa Aprili 4, 2021.

Ripoti za Shaban Makokha, Simon Ciuri na Wycliffe Nyaberi