• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 5:54 PM
Musalia arai Oparanya ahamie upande wake

Musalia arai Oparanya ahamie upande wake

Na DERICK LUVEGA

KIONGOZI wa chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, amemrai Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya ajiunge naye ili kumzuia kiongozi wa upinzani Raila Odinga, kupenyeza katika eneo la Magharibi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Bw Mudavadi pia anawataka wanasiasa wengine kutoka eneo hilo wanaomuunga Naibu Rais William Ruto, kuungana naye kuimarisha umoja wa jamii ya Waluhya nyuma yake.

Bw Mudavadi alisema kwamba ushindi wa chama chake kwenye uchaguzi mdogo wa eneobunge la Matungu na ule wa chama cha Ford Kenya eneobunge la Kabuchai, Kaunti ya Bungoma, ni ishara kwamba eneo hilo halijagawanyika kisiasa kama linavyodhaniwa.

Bw Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetangula, wanaendesha juhudi za kuwafungia nje Dkt Ruto na Bw Odinga kupenyeza katika eneo la Magharibi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Hii ndiyo sababu, Bw Mudavadi analenga kumvuta Bw Oparanya ambaye aliongoza kampeni za ODM Matungu, upande wake. Mgombeaji wa chama cha ODM, Bw David Were alikuwa wa pili katika uchaguzi mdogo wa Matungu kwa kupata kura zaidi ya 10,000, ushindi ukitwaliwa na Bw Peter Nabulindo wa ANC.

Kampeni za uchaguzi huo ambazo zilikuwa na ushindani mkubwa, zilionekana kuwa za ubabe kati ya Bw Mudavadi na Bw Oparanya.

“Tunawaalika marafiki wetu katika ODM na vyama vingine kujiunga nasi,” alisema Bw Mudavadi akisherehekea ushindi wake eneo bunge la Matungu.

Aliongeza, “Wakati umefika kwenu kutambua kwamba tunaweza kuafikia mengi tukiungana. Kama tungekuwa tumeungana tunavyopaswa, tunaweza kufanya makubwa,” alieleza.

“Namhimiza Gavana wa Kakamega Oparanya kuungana nami ili tuweze kushirikiana pamoja. Kama tunaweza kuungana pamoja kikamilifu, tunaweza kuafikia mengi,” aliongeza Bw Mudavadi.

Bw Mudavadi na Bw Oparanya wanataka kumrithi Rais Uhuru Kenyatta ambaye kipindi chake cha pili cha urais kinamalizika mwaka ujao. Lakini Dkt Ruto na Bw Odinga wamekuwa wakizuru eneo hilo kuwarai wapigakura.

Bw Mudavadi amewahi kusema kwamba eneo hilo linakumbatia demokrasia kwa kuwa limepigia kura wagombeaji kadhaa wa urais katika chaguzi zilizopita.

Hata hivyo, wakati huu, kiongozi huyo wa chama cha ANC anajitahidi kuunganisha eneo hilo nyuma yake baada ya kushirikiana kisiasa na Bw Wetang’ula, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na Bw Gideon Moi wa chama cha Kanu.

Katika tamko lililochukuliwa kuwalenga Bw Odinga na Dkt Ruto, Bw Mudavadi alisema: “ Kuna watu ambao wamekuwa wakitumia migawanyiko yetu kama jamii.”

Kuna minong’ono katika kambi ya Bw Mudavadi kwamba Bw Odinga anamtumia aliyekuwa waziri wa biashara, Dkt Mukhisa Kituyi agombee urais ili kugawanya kura za jamii ya Waluhya.

You can share this post!

Wanasiasa waanza kushtakiwa kwa vurugu chaguzini

Mke wake Mwanamfalme adai alibaguliwa sababu ya rangi