• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Matatizo ya CBC yatatuliwe upesi

TAHARIRI: Matatizo ya CBC yatatuliwe upesi

KITENGO CHA UHARIRI

MITIHANI ya kitaifa kwa wanafunzi wa Gredi Nne ilianza Jumatatu kwa changamoto tele katika shule mbalimbali nchini.

Mitihani hiyo ni mojawapo ya hatua kubwa ambazo zimechukuliwa kufikia sasa katika mpango wa kutekeleza mfumo mpya wa elimu wa CBC, na kufutilia mbali 8-4-4.

Imekuwa kawaida wakati wowote wa kutekeleza jambo jipya katika CBC huwa changamoto zinashuhudiwa.

Hapo jana, changamoto kuu iliyotajwa na walimu wengi katika pembe tofauti za nchi ni kuhusu ukosefu wa intaneti.

Hii ni kutokana na kuwa, walimu walitakikana kupata mitihani katika mtandao wa Baraza la Mitihani ya Kitaifa (KNEC).

Ukosefu wa intaneti hasa katika shule za mashambani ulifanya baadhi ya shule kuahirisha mitihani yao.

Ijapokuwa maafisa wa serikali wameondolea wadau wasiwasi kuhusu suala hili na kusema mitihani inaweza hata ikaandikwa ubaoni kwa kutumia karatasi ya shule jirani, hili si suala linalostahili kupuuzwa.

Wengi wetu hushuhudia jinsi wanafunzi katika shule za mijini wamekuwa wakitegemea mitandao ya intaneti kufanya kazi za ziada chini ya mtaala huu wa CBC.

Yale yaliyoonekana Jumatatu ni thibitisho tosha kuwa watoto wanaoishi mashambani wamekuwa wakikosa kujielimisha sawa na wenzao wa mijini.

Hili ni jambo ambalo linafaa kuchukuliwa kwa uzito kwani mojawapo ya malengo yaliyotajwa na serikali ilipoanza kutekeleza mfumo mpya wa elimu ni kuwa kuna lengo la kuleta usawa miongoni mwa watoto wote kitaifa.

Ni jukumu la serikali kuwezesha mashirika ya huduma za mawasiliano kitekinolojia kufikisha huduma hizo kote nchini.

Serikali ina uwezo wa kusambaza huduma hizo, lakini ukosefu wa moyo wa kujitolea miongoni mwa viongozi wa kisiasa wanaostahili kutoa sera mwafaka na wale wa taasisi husika wanaofaa kusimamia huduma hizo, ni pigo kubwa.

Safari ya kuleta usawa katika elimu itakuwa na changamoto tele. Huenda ikachukua miaka mingi kabla ikamilishwe.

Hata hivyo, kipindi hicho kitafupishwa kama tutakuwa taifa ambalo hujifunza kutokana na changamoto zake.

Huwa ni aibu jinsi kila mara tunakumbwa na changamoto zile zile ambazo tulishuhudia miaka iliyopita. Itakuwa aibu kama siku za usoni tutaendelea kushuhudia changamoto hizi tunazopitia sasa katika CBC.

You can share this post!

Mke wake Mwanamfalme adai alibaguliwa sababu ya rangi

ODONGO: Tishio kwa handisheki ni tishio kwa amani nchini