• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 1:08 PM
Pep aridhishwa na rekodi ya Man-City kwenye vita vya kutetea ufalme wa mataji ya EPL

Pep aridhishwa na rekodi ya Man-City kwenye vita vya kutetea ufalme wa mataji ya EPL

Na MASHIRIKA

KOCHA Pep Guardiola wa Manchester City amewasifu wanasoka wake kwa kuweka rekodi ya kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) miongoni mwa vikosi viwili vya kwanza jedwalini kila baada ya kutwaa taji la kipute hicho.

Mabingwa watetezi Liverpool sasa wako nje ya mduara wa nne-bora, katika nafasi ya nane kwa alama 43, huku pengo la alama 22 likitamalaki kati yao na viongozi Man-City.

Man-City ndicho kikosi cha pekee tangu mwaka wa 2012 kuwahi kukamilisha kampeni za EPL ndani ya orodha ya nne-bora baada ya kunyanyua ubingwa katika msimu uliotangulia.

“Mashabiki wetu hututia presha ya kufanya vyema na kupigania ufalme wa kila shindano tunaloshiriki kila msimu,” akasema kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich.

Tangu watawazwe mabingwa wa EPL kwa mara ya kwanza mnamo 2011-12, Man-City wamekamilisha kampeni za kivumbi hicho kwenye kila mmojawapo ya msimu katika nafasi ya pili kwa misimu mitatu mfululizo kabla ya kutwaa ufalme mnamo 2017-18 na kulihifadhi taji hilo mnamo 2018-19 chini ya Guardiola ambaye ni raia wa Uhispania.

Manchester United walitupwa hadi nafasi ya saba mwaka mmoja baada ya kutwaa taji la EPL mnamo 2013 huku Chelsea wakiambulia nafasi ya 10 na tano msimu mmoja baada ya kutawazwa mabingwa.

Leicester City kwa upande wao walitupwa hadi nafasi ya 12 msimu mmoja tu baada ya kuibuka mabingwa wa EPL mnamo 2015-16 chini ya kocha Claudio Ranieri ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya Sampdoria katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

“Kitu kizuri zaidi ambacho Man-City wamefanya ni kusalia miongoni mwa washindani wakuu wa taji la EPL pindi baada ya kutwaa ufalme katika msimu uliotangulia,” akasema Guardiola ambaye ameongoza kikosi chake kushinda jumla ya mechi 20 kati ya 28 zilizopita katika mashindano ya EPL msimu huu.

Ni pengo la pointi 11 ndilo kwa sasa linatamalaki kati ya Man-City na nambari mbili Man-United iliyoongozwa na kocha Ole Gunnar Solskjaer kutandika masogora wa Guardiola 2-0 kwenye Debi ya Manchester mnamo Machi 7, 2021 ugani Etihad.

Man-City hawajawahi kukamilisha kampeni za EPL nje ya mduara wa nne-bora tangu msimu wa 2009-10 walipoanza msimu chini ya kocha Mark Hughes na hatimaye kukamilisha kampeni za muhula huo katika nafasi ya nne.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mabadiliko ya makamanda wa polisi yafanyika Makadara

Aliyekuwa afisa wa mechi ya UEFA iliyotibuka kati ya PSG na...