Madhara yaletwayo na uvaaji wa viatu vyenye visigino virefu kwa mjamzito

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

KIPINDI cha ujauzito ni wakati wa kubadili mambo mengi katika mfumo wa maisha ya mwanamke.

Moja ya mambo makubwa ni pamoja na tabia ya kuvaa viatu vyenye visigino virefu.

Mjamzito anashauriwa kuepuka viatu vyenye visigino virefu kutokana na athari zinazoweza kutokana na aina hizi za viatu, kama ifuatavyo.

Maumivu ya misuli ya mapaja

Kina dada hupenda kuvaa “high heels” na hali hii husababisha misuli ya mapaja kukaza na kuwa na ‘mwonekano mzuri’. Katika kipindi cha ujauzito, mabadiliko ya homoni husababisha misuli hii kuwa na maumivu tofauti na hali ilivyokuwa kabla ya ujauzito.

Maumivu ya mgongo

Wakati wa ujauzito, uzito mkubwa huhamia mbele na misuli ya nyonga hulegea. Mabadiliko haya ya kimsawazo huweza kusababisha maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo na kiuno.

Hatari ya kuanguka

Ni wazi kuwa uzito huongezeka wakati wa ujauzito na mabadiliko ya vichocheo vya mwili husababisha kizunguzungu cha hapa na pale. Hii huongeza hatari ya kuanguka iwapo utavaa “high heels” na hivyo hatari ya kupata majeraha kwako na kwa mtoto aliyeko tumboni.

Uvimbe miguuni

Ni jambo la kawaida miguu kuvimba wakati wa ujauzito. Kuvaa viatu vyenye visigino virefu na vyenye kubana huweza kuongeza tatizo hilo na kupelekea maumivu.

Mimba kutoka

Mjamzito akivaa viatu vyenye visigino virefu anakuwa katika hatari kubwa ya kuanguka. Hii huweza kusababisha majeraha makubwa kwa mtoto aliyeko tumboni hali inayoweza kusababisha mimba kutoka.

Lakini, iwapo kuna ulazima sana wa kuvaa viatu hivyo, unapaswa kuzingatia mambo mbalimbali. Ni salama kuvaa viatu hivi katika muhula wa kwanza wa ujauzito (miezi mitatu ya mwanzo), viatu visiwe virefu sana na visigino viwe imara, lakini pia ni muhimu kuvaa viatu visivyo kukaza sana.

Ni vyema kuepuka visigino vyembamba sana na si siku nzima; vitoe mara kwa mara kupumzisha miguu.

Epuka kutembea au kusimama muda mrefu ukiwa umevivaa. Endapo utahisi maumivu kwenye misuli ya mapaja, jaribu kufanya mazoezi ya kujinyoosha na kujikanda.